Uamuzi wa kuongeza muda hapana shaka ni mwitikio wa kilio cha wadau
wengi wa uchaguzi mkuu kwamba wananchi wengi wa mkoa huo walikuwa
hawajajiandikisha licha ya taarifa ya Nec kuonyesha kuwa hadi juzi,
waliokuwa wamekwisha kuandikishwa ni wapigakura milioni 1.7 kati ya
lengo la kuandikisha wapiga kura milioni 2.9 kwa mkoa huo.
Kimahesabu hadi siku mbili zinabakia kukamilika kwa kazi ya
uandikishaji kwa kufuata ratiba ya awali, Nec ilikuwa imefanikiwa
kufikia lengo lake kwa walao asilimia 58.6. Mafanikio haya siyo mazuri
sana hata kama kungefurika maelfu ya watu vituoni kwa siku hizo mbili.
Isingeliwezekana kuandikisha watu milioni 1.2 kwa siku mbili tu. Uwezo
huo haupo.
Ndiyo maana tunachukua fursa hii kuipongea Nec kwa kuwa sikivu,
hivyo kuongeza muda wa kuandikisha wapiga kura katika mkoa wa Dar es
Salaam kwa siku nne zaidi. Tunaamini hatua hii itakuwa ni fursa murua
kwa wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi zaidi ili ifikapo Jumanne ya
Agosti 4, mwaka huu walao lengo liwe limefikiwa na ikiwezekana kuvuka.
Pamoja na usikivu wa Nec, sisi bado tuna maswali, hoja na tashwishi
nyingi kwamba bado kuna mambo mengi hayajakaa sawa katika mchakato
mzima wa uandikishaji wapiga kura. Kubwa ya yote ni uwezo wa mashinde za
BVR na pengine hata uwezo wa waandikishaji wenyewe.
Tangu kuanza kwa kazi ya uandikishaji wapigakura Februari 23, mwaka
huu mkaoni Njombe kumekuwa na changamoto za kiufundi ambazo zingali
zinaendelea kuwako hata sasa katika mkoa wa Dar es Salaam licha ya
uzoefu ambao umepatikana katika mikoa mingine yote ya nchi ambako kazi
hii imekamilika.
Kuzimika ovyo kwa mashine hizi ni mambo ya kawaida kabisa. Katika
baadhi ya vituo kuna mashine zinazimika hadi nusu saa. Zikiwashwa
zinachukua muda mrefu sana kuwaka huku wananchi wakitaabika juani
wakisubiri kuandikishwa.
Maeneo mengi katika mkoa wa Dar es Salaam kumekuwa na msongamano au
tuseme misururu mirefu ya wananchi wanaodamka alfajiri na mapema
wengine hadi saa tisa, ili kuwahi kupata namba kwenye vituo. Wapo
wanaoandikishwa baada ya kusota vituoni siku mbili hadi tatu.
Tunafikiri, Nec ilikuwa na uwezo wa kuwa na vituo vingi kadri
iwezekanavyo na kuongeza mashine za BVR nyingi zaidi kwa kuwa zipo za
kutosha kwani maeneo mengine ya nchi kazi ya uandikishaji imekwisha
kukamilika.
Kwa kutambua ukweli huo, haitoshi tu kwa Nec kuongeza muda wa siku
nne ili wananchi zaidi wajiandikishe kama idadi ya mashine itaendelea
kubakia ilivyo sasa. Nguvu kubwa zaidi ya vifaa na watendaji vituoni
inatakiwa ili kufanikisha kazi hii muhimu.
Ni fedheha kwa wananchi kudamka alfajiri kiasi hicho, lakini
mwishoni washindwe kujiandikisha kwa sababu tu ya uhaba wa mashine
vituoni, au kwa sababu tu zinazimika zimika kila mara kwa sababu yoyote
ile. Nec inapaswa kuondoa kasoro hii.
Wananchi wamesikia tamko la Nec kwamba sasa vituo vya kuandikisha
wananchi vifunguliwe kuanzia saa 1:00 asubuhi na kuendelea kufungwa saa
12:00 jioni, lakini swali gumu ambalo halina majibu ni je, makarani hao
wanaofanya kazi ya kuandikisha watu watafika vipi kwenye vituo vyao? Je,
Nec imeweka utaratibu gani wa usafiri wa kuwawezesha kufika kwenye
vituo? Tunajua wapo wanaokaa mbali na vituo vyao, lakini pia maeneo
mengine ambako vituo vimewekwa hakuna usafiri wa umma. Huko kote
kunahitaji nguvu ya Nec kuwezesha kazi kuanza saa 1:00 asubuhi.
Pamoja na changamoto hii kwa Nec, tunaamini kwamba wakazi wa Dar es
Salaam ambao hawajajiandikisha kwa sababu yoyote ile nao watawajibika
kutumia siku hizo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili ifikapo Oktoba
25, mwaka huu watumie haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wao. Ni
matumani yetu kwamba Nec wataendelea kutafutia ufumbuzi changamoto hizi
kwa upande mmoja, lakini kwa upande mwingine wananchi wataendelea
kujitokeza kwa wingi zaidi kujiandikisha katika siku hizo nne
zilizoongezwa na hatimaye watumie haki yao ya kidemokrasia Oktoba 25,
mwaka huu kuchagua madiwani, wabunge na rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
0 comments:
Post a Comment