Kitendo cha wagombea hao kugomea kusaini matokeo ya uchaguzi, kilitokea muda mfupi baada ya msimamizi wa uchaguzi kumtangaza, mbunge wa Viti Maalum anayemaliza muda wake, Felister Bura, kuwa mshindi wa uchaguzi huo.Bura alipata kura 457 dhidi ya wapinzani wake 21, akiwamo aliyewahi kuwa waziri wa maliasili na utalii, katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete, Shamsa Mangunga.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, katibu wa umoja wa wanawake wa CCM (UWT), mkoani Dodoma, Kaundime Kasase, alidai kuwa Mwangunga aliambulia kura 25 kati ya 728 zilizopigwa.
Katika uchaguzi huo, walitakiwa kupatikana wawakilishi katika makundi manne: Wabunge wawili wa mkoa, mbunge mmoja kutoka kundi la watu wenye ulemavu, wafanyakazi, wasomi na asasi zisizokuwa za kiserikali.
Katika kinyanyiro hicho cha kuwapata wawakilishi wawili kutoka mkoa, mshindi alikuwa Bura akifuatia Fatuma Toufiq, ambaye ni mkuu wa wilaya ya Manyoni aliyepata kura 368.
Kupitia kundi la watu wenye ulemavu, msanii wa muziki wa kizazi kipya, Khadija Shaaban maarufu kwa jina la Keisha aliibuka mshindi katika kundi hilo. Alipata kura 340.
Katika kundi la wasomi, Juliana Manyerere, ndiye aliyeibuka kidedea; kundi la asasi zisizo za kiserikali akiibuka Chiku Mugo; huku kundi la wafanyakazi, aliyetangazwa mshindi alikuwa mwalimu wa shule ya Msingi Kizota, Mwanamanga Mwanduga.
Akizungumza na MwanaHALISI Online, mmoja wa wagombea aliyesusia matokeo ya uchaguzi huo, Neema Majule alisema, uchaguzi mzima uligubikwa na rushwa na ukiukwaji wa maadili.
“Vitendo vya rushwa vilikuwa vinaendelea nje ya ukumbi wa uchaguzi. Baadhi ya wapambe walikuwa wanatoa rushwa chooni. Nilitoa taarifa kwa mmoja wa maafisa usalama waliokuwepo katika ukumbi huo ambapo aliweza kwenda kufunga milango ya choo ili watu wasiweze kujificha huko,” anaeleza.
Aidha, Majule anasema, hakuna aliyeweza kuamini matokeo hayo kutokana na mpishano wa kura uliopo katika kura na matokeo yaliyotangazwa na hivyo, kuvitaka vitakavyosikiliza malalamiko yao kutenda haki.
Naye Judith Mieya alisema, wamegoma kusaini matokeo hayo kwa kuwa yalitokana na rushwa na kwa hali wamegoma kukubaliana na vitendo vya utovu wa nidhamu katika chama chao.
“…jambo hilo (rushwa) limekuwa likikemewa siku zote. Isingekuwa vyema kukubaliana na matokeo ambayo yametokana na vitendo vya rushwa. Tunategemea suala hilo litafikishwa katika vikao husika liweze kujadiliwa kwa mujibu wa kanuni za chama hicho.
Akijibu malalamiko hayo, Kasase alisema, hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hajapokea rasmi malalamiko ya wagombea hao.->http://mwanahalisionline.com
0 comments:
Post a Comment