Katibu
wa CCM Wilaya ya Mjini Ndg Mohammed Omar Nyawanga akisoma Tamko la Mikoa Mnne
ya CCM Unguja kuhusuana na Mhe Edward Lowassa. kwa Waandishi wa habari na
Makada wa CCM Afisi Kuu ya CCM Zanzibar leo.
NDUGU WANAHABARI!
ASALAM ALEYKUM!
Awali ya yote, kwa niaba ya
Wanachama na Makada wenzangu tuliokusanyika hapa leo, ninapenda kuchukua fursa
hii kumshukuru Molla wetu mtukufu mwingi wa rehemu kwa ukarimu wake na
kutujaalia afya njema na uwezo wa kukutana nanyi hapa leo. Pili ninapenda
kuwashukuru kwa dhati Wahariri na Wanahabari kutoka Vyombo mbali mbali vya
Habari vya hapa Zanzibar, kwa kukubali kuitika wito wetu huu maalumu.
Sisi tuliowaita hapa ni Wanachama na
Makada wa CCM. Baadhi yetu ni viongozi wa CCM wa ngazi mbali mbali za
Chama, wakiwemo Wajumbe wa Halmashauri Kuu za CCM za Wilaya, Mikoa na Taifa.
Kwa kuzingatia nasabu yetu hio, ndio maana mkutano huu tumeamua kuufanyia
katika jengo letu hili la Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.
Lengo kubwa la kuwaiteni hapa leo,
ni kuwaelezea hisia na msimamo wetu kama wanachama na viongozi wa CCM ambao kwa
kuzingatia wajibu na majukumu tuliyonayo katika Chama, sisi ndio wasimamizi
wakuu wa Siasa, Sera na Itikadi ya CCM hapa Zanzibar.
Hivyo basi, kwa kuzingatia hali ya
Kisiasa iliyojiri hapa nchini, tangu kumalizika kwa Mkutano Mkuu Maalumuwa CCM
wa Taifa uliofanyika tarehe 12 na 13/7/2015 mjini Dodoma, na kumchagua Mhe.
Dk. John Pombe Joseph Magufuli kuwa mgombea wa CCM wa Kiti cha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumthibitisha Mhe. Samia Suluhu Hassan
kuwa mgombea mwenza na uhusika wetu katika maamuzi hayo ya Chama, tumeona ipo
haja na umuhimu mkubwa wa kuitisha mkutano huu na kupitia kwenu kuwaeleza
wanachama wenzetu wa CCM na Watanzania kwa jumla, hisia na muono wetu juu ya
mustakabali wa Chama chetu na hatima ya Taifa letu.
Kama tunavyofahamu mapema mwezi Mei
2015, Chama chetu kilitangaza ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM
katika chaguzi za Vyombo vya Dola. Ratiba hio ilihusu uteuzi wa mgombea
wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar pamoja na Madiwani.
Mchakato
wa uteuzi wa wagombea wa CCM wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Rais wa Zanzibar, ulianza tarehe 3/6/2015 hadi 2/7/2015, kwa
wanachama kuchukua na kuresha fomu za maombi. Baada ya hapo vikao vya
uchujaji vilianza kuanzia tarehe 4/7/2015 na kumalizika tarehe 13/7/2015.
Jumla ya Wanachama wa CCM 42 walijitokeza kuchukua fomu za maombi na kati yao
38 walifanikiwa kukamilisha masharti yaliyotakiwa na kurejesha. Miongoni
mwao walikuwemo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri Wakuu Wastaafu, Mawaziri,
Majaji Wakuu Wastaafu, Mabalozi, Mawaziri na hata wanachama wa CCM wa
kawaida tu (wakulima, wafugaji n.k).
Kwa kuzingatia Katiba na Kanuni za
Chama chetu, kikao cha kwanza kabisa cha uchujaji wa wagombea ni Kamati ya
Usalama na Maadili ya ngazi husika. Hivyo, kwa wagombea wa Kiti cha
Rais, Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa ndicho chombo cha kwanza kabisa
chenye wajibu wa kuchambua kwa makini ubora wa wanachama wanaoomba Uongozi, ama
viongozi wanaoteuliwa katika ngazi mbali mbali za Chama, kabla vikao
vinavyohusika havijatoa idhini ya kuwaruhusu wateuliwe kugombea uongozi huo ama
kushika nafasi zilizo kusudiwa.
Kikao cha pili ni Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, ambayo chini ya ibara ya 119(6)(b) ya Katiba
ya CCM ya mwaka 1977, Toleo la 2012, imepewa jukumu la kufikiria na kutoa
mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya majina ya wanachama
wasiozidi watano wanaoomba kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Ndugu Wanahabari!
Tumelazimika kuvinukuu vifungu hivyo
vya Katiba na Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM, kwa sababu huo ndio msingi
uliofuatwa na Chama chetu katika uteuzi wa Wagombea wa Kiti cha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na maelezo ya baadhi ya watu wasioitakia
mema CCM na kwa kuzingatia maslahi yao binafsi wanataka kuwaaminisha Watanzania
kwamba, mchakato huo uligubikwa na mizengwe, chuki na kila aina ya ubabaishaji,
jambo ambalo sio la kweli.
Tunayasema haya sio kwa ushabiki
wala kushawishiwa na mtu au kiongozi yeyote wa CCM. Bali ukweli ni kwamba
sisi wenyewe tulikua sehemu ya mchakato huo na tulishiriki katika kila hatua ya
utekelezaji. Na kama ni kushawishiwa basi baadhi yetu tulishawishiwa
kumuunga mkono huyo ambaye leo analalamika kuwa, CCM haikumtendea haki.
Sio siri, baadhi yetu tulikubali kumsaidia na kufanya kampeni kubwa ya kuwaomba
wanachama wenzetu wa CCM wakubali kumdhamini katika Mikoa mbali mbali ya
nchi yetu. Tulifanya hivyo tukifahamu vyema matakwa ya Katiba na Kanuni
za Chama chetu kwamba, mwisho wa siku vikao halali vya Chama ndio vyenye wajibu
na mamlaka ya kufanya maamuzi kwa kuzingatia Katiba na Kanuni za Chama
chetu.
Hata hivyo, wengi hapa
hatujashangazwa hata kidogo na kwa kweli tulitegemea kuona kile kilichotokea tarehe
28/7/2015 kwa ndugu yetu Waziri Mkuu wa zamani, Kada na Kiongozi wa muda
mrefu wa CCM Edward Ngoyai Lowassa, kujitoa katika CCM na kujiunga na Chama cha
upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwa madai kwamba, CCM imeuonea
na haikumtendea haki!
Tunasema hivyo kwa sababu tulianza
kupata mashaka pale tuliposikia kauli zake wakati akijibu maswali ya baadhi ya
Waandishi wa habari kwamba, katika mchakato wa uteuzi wa mgombea wa CCM wa Kiti
cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya Chama, kwa upande wake
hakuna kushindwa wala kikao chenye uwezo wa kukata jina lake. Kimsingi,
kauli hio sio tu ni ya kukidhalilisha Chama chetu bali vile vile ni uasi!
Kwani ndugu Lowassa anafahamu vyema wajibu wa mwanaCCM na mamlaka ya kila kikao
ndani ya Chama. Iweje leo atamke tena hadharani kwamba, CCM ni lazima
imteue yeye kuwa mgombea wake na hakuna mwanachama mwengine ye yotemwenye
sifawala uwezo wa kumudu kuliongoza Taifa letu zaidi ya yeye tu peke
yake!
Aidha, ni jambo la ajabu sana kuona
kuwa, wale waliokua maadui zake wakubwa kisiasa,wakiwemo Viongozi Wakuu wa
Vyama vya upinzani ambao walizunguka ndani na nje ya nchi kulichafua jina lake
na CCM, leo hii bila haya wala soni ndio wanaosimama mbele ya Vyombo vya Habari
na kupaza sauti zao eti CCM imemuonea na kumdhalilisha Lowassa! Kama hio
haitoshi, wapo wale wanaodiriki kututisha, eti nyuma yake lipo kundi kubwa la
wanaCCM ambao wapo tayari kumfuata popote pale aendapo.
Ili kujibu madai hayo, na kwa
kupitia kwenu Waandishi wa Habari, tunapenda kutumia fursa hii kumueleza ndugu
Edward Ngonyai Lowassa pamoja na wote wanaomuunga mkono hususan Viongozi
na wanachama wa UKAWA, kwamba:-
a) Sisi
wote tuliyopo hapa leo na maelfu ya wanaCCM waliyo nyuma yetu hususan katika
Mikoa yote ya Zanzibar, tulimuunga mkono Lowassa katika azma yake ya kuomba
kuteuliwa na CCM kuwa mgombea wake wa Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, sio kwa sababu ya uzuri wa suara
yake au utajiri alionao hapana! Bali ni kwa sababu ya Siasa, Sera na Ilani ya
Chama alichokiamini na kukipigania, yaani CCM. Hivyo, kwa kuwa sasa
ameamua kujitenga na CCM, basi nasi tumeamua kujitenga naye na kamwe hatuko
pamoja naye.
b) CCM
ni muumini wa Haki za Binadamu, usawa na utawala wa sheria. Hivyo,
kujiondoa kwa Lowassa katika CCM ni sawa na ilivyokua wakati wa kujiunga
kwake. Ni suala la hiari yake na wala hatuna ugomvi naye. Ila
tunamkumbusha tu kwamba, inawezekana kabisa umaarufu alionao sasa umejengwa
kutokana na CCM, lakini haiwezekani kabisa kuwa, umaarufu wa CCM umejengwa au
kutokana na yeye. Ndio maana tunasema, Chama kwanza mtu baadae”.
c) CCM
ni Chama chenye mamilioni ya wanachama na maelfu ya viongozi, wenye hekima,
busara, mapenzi na uadilifu mkubwa kwa wananchi. Bado kinaamiwa na
kukubalika miongoni mwa wananchi wengi wa Tanzania. Wingi huo wa
wanachama wake haitokani na wala haujaletwa na utajiri wa Viongozi wake.
Bali unatokana na uimara wa Siasa, Sera na Itikadi yake., Hivyo, hasara
ya kweli kwa CCM sio kumpoteza tajiri mmoja anaetaka kubadili Sera na Itikadi
ya CCM kwa maslahi yake binafsi na marafiki zake, bali ni kuwapoteza mamilioni
ya wanachama wake ambao wanachoshwa na viongozi walafi na wanafiki ndani ya
CCM!
d) Kwa
kuzingatia ukweli huo ni wazi kwamba, uamuzi wa Lowassa kujiondoa ndani ya CCM
sio jambo la kukishtua Chama chetu, viongozi wala wanachama wake. CCM
kamwe haiwezi kudhoofika wala kupasuka. Aidha, hii sio mara ya kwanza kwa
CCM kuondokewa na Kiongozi Mwandamizi na kujiunga upinzani. Mwaka 1989,
CCM iliwafukuza uanachama jumla ya viongozi waandamizi 11 akiwemo Waziri
Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar, Seif Shariff Hamad. Akafuatia Agostino
Lyatonga Mrema, ambaye alijiunga na NCCR-Mageuzi. Mwaka jana 2014, CCM
ilimfukuza uanachama aliyekua Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki kwa tiketi ya
CCM Mansoor Yussuf Himid. Hivyo, kama wahenga walivyonena tunamuambia
Lowassa, “Kama mvuvi wa pweza tukutane mwambani” !
e) Tunawashangaa
sana Viongozi wa baadhi ya Vyama vya Upinzani hasa vile vinavyounda umoja wa UKAWA
na hususan Viongozi na Wanachama wa CHADEMA kwa namna wanavyoendelea kuendesha
Siasa za ubabaishaji na ulaghai kwa Watanzania. Kwa hakika ni jambo la
aibu na kufedhehesha sana kuona kwamba, hata baada kufikisha umri wa miaka 23,
tangu kuanzishwa rasmi kwa Vyama vya Upinzani hapa nchini (1992), bado Vyama
hivyo hadi leo hii vimeshindwa kuandaa wagombea wenye uwezo wa kuwaongoza
Watanzania na kuishia kudaka mapumba yanayotoka CCM?Mara nyingi tumewasikia
wakijitoa kimasomaso kwakukariri nusu nusu kauli ya Baba wa Taifa Hayati
Mwalimu Julius K. Nyerere kwamba, “Watanzania
wanahitaji mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayafuata nje ya CCM”.
Kwa bahati mbaya sana wasia huo wa Baba wa Taifa unakaririwa nusu nusu.Naomba
kuwakumbushaViongozi wa UKAWA kwamba, Wasia huo wa Baba wa Taifa kwa
Watanzania unaendelea kwa kutamka kwamba “Rais wa Tanzania anaweza kutoka
Chama cho chote kile, lakini Rais bora wa nchi yetu atatoka CCM!
Mwisho kabisa, ninapenda nimalizie
kwa kumpongeza sana Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuteuliwa kuwa
mgombea wa CCM wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia
Suluhu Hassan kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza, pamoja na wanachama wengine
wote waliojitokeza kutangaza nia hatimaye kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa
kugombea nafasi ya kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa
heshima kubwa waliyoipatia CCM na kubwa zaidi kwa kukubali kupokea bila
kinyongo maamuzi ya Chama na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa
wanaCCM.
0 comments:
Post a Comment