TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) pamoja na vyama vya siasa 22 imepitisha maadili yatakayotumika katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Pia vyama vya siasa vimeshinikiza kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi
(IGP), awe sehemu ya maadili hayo kuepuka jeshi lake kunyanyasa viongozi
na wafuasi wa vyama vya siasa.
Katika mkutano wa kujadili maadili hayo jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji
Damian Lubuva alisema maadili hayo yatahusisha zaidi vyama vya siasa,
wagombea wote, Serikali pamoja na Tume yenyewe, jambo ambalo viongozi wa
vyama vya siasa walisema kwa upande wa Serikali, anayehusika zaidi ni
IGP.
Maadili hayo yanavitaka vyama vya siasa na wagombea wake kuheshimu,
kutekeleza sheria za uchaguzi, kanuni, maadili na sheria nyingine za
nchi katika kipindi chote cha uchaguzi yaani kuanzia kampeni hadi siku
ya uchaguzi.
Mawaziri, watendaji
Kwenye maadili hayo, mawaziri wametakiwa wasichanganye ziara za
kikazi na shughuli za kiuchaguzi na wasitumie vyombo au watendaji wa
Serikali katika shughuli za uchaguzi kwa manufaa yao.
Kuanzia kipindi cha kampeni, mawaziri na watendaji wengine wa
Serikali hawatakiwi kutangaza katika vyombo vya habari au kwa namna
yoyote misaada au ahadi ya aina yoyote, kutoa ahadi za shughuli za
maendeleo ya jamii kwa mfano kujenga barabara, kusambaza maji na
wasitumie rasilimali za umma kwa shughuli za kampeni.
Maadili hayo pia yanaeleza mambo ambayo hayatakiwi kufanywa na vyama
vya siasa na wagombea, mambo yanayotakiwa kufanya au kutofanywa wakati
wa upigaji kura mpaka kutangaza matokeo ya uchaguzi, wajibu wa Serikali
na Tume ya Uchaguzi.
Miongoni mwa mambo ambayo yanakatazwa na maadili hayo ni wafuasi wa
vyama vya siasa kufanya fujo au kusababisha vurugu ya aina yoyote katika
mkutano wa chama kingine cha siasa.
Wafuasi vituoni
Pia wafuasi wa vyama vya siasa, wametakiwa kuondoka vituoni mara tu
baada ya kupiga kura, ili kuepusha msongamano na vitendo vingine
vinavyoweza kuchochea kuvunjika kwa amani.
Jaji Lubuva pia alisema maadili hayo yanaitaka Serikali wakati wa
uchaguzi kutoa fursa sawa kwa wadau wote, ikiwemo vyama vya siasa, ili
kuviwezesha kuendesha shughuli zao za kisiasa kwa kuzingatia sheria za
nchi, ikiwemo kuruhusu wagombea urais kutumia vyombo vya habari vya umma
katika kutangaza sera zao.
Aidha mawakala wa vyama vya siasa, wamezuiwa kutumia simu za
viganjani wawapo katika kituo cha kupiga kura, kwa kuwa waliohudhuria
wametamkwa kabisa katika maadili hayo.
Goli la mkono
Hata hivyo, mkutano huo nusura uingie dosari, baada ya baadhi ya
viongozi wa vyama vya siasa kuonesha wasiwasi wao kuwa maadili hayo
hayana maana, kwani tayari CCM kupitia kwa baadhi ya viongozi wao
wameshaapa kuwa watashinda hata kwa goli la mkono.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema kama maadili hayo
yanataka vyama vyote kufuata sheria, inakuwaje Katibu wa Halmashauri Kuu
ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ajitape kuwa
lazima chama chake kitashinda hata kwa goli la mkono na NEC yenyewe
imekaa kimya.
“NEC mko kimya, IGP yuko kimya na msajili ya vyama vya siasa yuko
kimya, hivi kweli hapo kuna haki itatendeka, je haya maadili ni mapambo?
Alihoji Dk Slaa.
Dk Slaa pia alihoji inakuwaje wanaenda kujadili maadili wakati hata
sasa mgawanyo wa majimbo haueleweki jambo ambalo limefanya kuwe na
vurugu ndani ya vyama vya siasa. Alihoji tume inasubiri nini kutangaza
majimbo hayo mapya.
Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi naye alisema maadili
hayo hayana maana kama chama tawala kimeanza kutoa kauli ambazo
zinaonesha kuwa wamejipanga kuvuruga uchaguzi, jambo ambalo linakatazwa
na maadili hayo.
“Hapa tunafanya nini kama chama tawala kimeshaanza kutoa kauli hizo
halafu mnataka mtuaminishe kuwa uchaguzi utakuwa huru na haki,” alisema
Dk Makaidi.
NEC yajitenga
Hata hivyo Jaji Lubuva alisema maadili hayo yanahusika siku ya kwanza ya kampeni hadi siku ya kupiga kura na kutangaza matokeo.
Alisema tume yake haihusiki na kauli hizo kwani hawana mamlaka
yanayowapa kulizungumzia mambo ambayo yako nje ya sheria ya uchaguzi.
“Kuna vyombo vingine vinavyoshughulika na nyinyi kabla ya kampeni,
sisi tunahusika wakati wa kampeni tu, hivyo hayo mengine hayatuhusu,”
alisema Jaji Lubuva.
Kuhusu majimbo mapya, Jaji Lubuva alisema bado wako kwenye mchakato
wa kukamilisha kuunda majimbo hayo mapya na hivi karibuni watatangaza na
kuwataka viongozi wa vyama vya siasa kuwa na subira.
IGP na maadili
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula pamoja na Dk Slaa, ndio
waliotoa hoja ya kutaka IGP awemo kwenye maadili hayo ili kuepusha
malalamiko kutoka kwa wanasiasa hao kuwa jeshi hilo linakwepa
kushughulika na kesi za kisiasa.
Dk Slaa katika hoja yake alisema katika uchaguzi uliopita, walipata
shida na polisi kwani kila walipokuwa wanapeleka kesi zinazotokana na
kampeni, polisi walikwepa kuwa hawashughuliki na masuala ya kisiasa.
Mangula kwa upande wake alisema anaunga mkono hoja ya Dk Slaa kuwa
IGP lazima naye awe sehemu ya maadili hayo, ili kuondoa malalamiko ya
wanasiasa na ajue namna atakavyowajibika wakati wote wa kampeni za
uchaguzi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment