Kuanza kwa michuano hiyo kipindi hiki ambacho madirisha ya usajili
sehemu mbalimbali duniani yakiwa wazi, ni faraja kubwa kwa wachezaji
wanaoshiriki kinyang'anyiro hicho kwani kunaweza kuwafungulia milango
kwa kusajiliwa na klabu kubwa ndani na nje ya ukanda huu wa Cecafa.
Kiwango na nidhamu kwa wachezaji ndiyo sifa pekee itakayozishawishi
na kuzivutia klabu kuwekeza kwao, hivyo wachezaji hawana budi kujituma
zaidi huku wakifahamu kuwa wako sokoni na mawakala wanawafuatilia.
Tunaamini kutakuwapo na mawakala mbalimbali ambao watakuwa 'bize'
kusaka vipaji kwa ajili ya msimu mpya, hivyo soko la wachezaji
watakaoonyesha kiwango ni dhahiri kwa sasa ni kubwa kupitia michuano
hiyo.
Mbali na uwapo wa mawakala, pia kitendo cha michuano hiyo
kuonyeshwa 'laivu' kupitia Kituo cha SuperSport, kunaongeza wigo zaidi
kwa wachezaji watakaonyesha kiwango kuonekana sehemu mbalimbali duniani.
TAMBARARE tukiwa kama mdau namba moja wa michezo, tunatamani kuona
wachezaji wengi ukanda huu hususan wa Tanzania wakipata nafasi ya
kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kwani kwa kufanya hivyo kutazidi
kuiimarisha timu yetu ya Taifa, Taifa Stars.
Hatutarajii kuona utovu wa nidhamu kama ulioonyeshwa na
mshambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe Donald Ngoma, katika mechi dhidi ya Gor
Mahia ya Kenya, ukiendelea kwani mbali na kuigharimu timu yake pia hiyo
si picha nzuri katika soko la soka.
Muamuzi Ssali Mashood wa Uganda alilazimika kumuonyesha kadi ya
pili ya njano Ngoma katika dakika ya 23 baada ya kumsukuma kwa ghadhabu
Haruna Shakava aliyekuwa amemuangusha, wakati kadi ya kwanza Mzimbabwe
huyo aliipata kutokana na kosa la kumvuta jezi Sibomana Abouba aliyekuwa
amemuacha nyuma mwanzoni mwa mchezo huo wa Kundi A.
Sote tunatambua kuwa Ngoma ni mchezaji mzuri na mwenye kipaji cha
soka na anayeweza kuzivutia klabu kubwa, lakini anapaswa kubadilika kwa
kuonyesha nidhamu zaidi mchezoni, vinginevyo hilo linaweza kumpotezea
nafasi ya kujiuza klabu kubwa.
Tunaamini mchezaji anayejitambua hana budi kukilinda kipaji chake
kwa kuwa na nidhamu kwani hicho ni moja ya kigezo kikubwa katika soko la
soka.
Tunatambua kuwa kupitia michuano hiyo ya Kagame, mchezaji anaweza
asipate soko kwa wakati huu lakini akawa amejifungulia milango kwa
kuanza kufuatiliwa kipaji na nidhamu yake nje na ndani ya uwanja na
mawakala.
Katika hilo, mfano mzuri ni Mrisho Ngasa aliyesajiliwa na Klabu ya
Free State Stars inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini, baada ya kocha
wa timu hiyo Mmalawi Kinnah Phiri kukiri kuwa alikuwa akimfuatilia kwa
muda mrefu wakati akiichezea Taifa Stars na klabu yake, hivyo
kuridhishwa na kiwango cha winga huyo ambaye amepanga kumchezesha kama
mshambuliaji.
Ni wazi kabisa baada ya kuridhishwa na uwezo wa Ngasa, nidhamu
mchezoni ni moja ya mambo ambayo Phiri alivutiwa nayo hasa ukizingatia
ukweli kwamba winga huyo hana historia ya nidhamu mbaya ndani ya
uwanja.
Kadhalika ni aibu kuona mchezaji ambaye maisha yake yanategemea
soka kushindwa kulinda kipaji chake kutokana na kuwa na nidhamu mbaya
katika kazi yake inayomfanya kumudu kuendesha maisha yake ya kila siku.
Tayari Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm ameonyesha
kukerwa na nidhamu mbaya aliyoonyesha Ngoma baada ya kueleza kuwa
mshambuliaji huyo ndiye aliyeikosesha ushindi timu yao kutokana na
kutolewa mapema na hivyo kuwafanya wacheze pungufu takribani dakika 65.
Pluijm alisema unapokuwa tayari umeshaonyeshwa kadi ya njano, ni
lazima ucheze kwa tahadhali maana muda wowote unaweza kuigharimu pakubwa
timu yako huku pia akilalamika kumkosa Ngoma katika mechi ya Jumatano
dhidi ya Telecom, kutokana na kuwa nje akitumikia adhabu hiyo ya kadi.
TAMBARARE tunaamini kuna haja ya makocha kusisitiza nidhamu kwa
wachezaji kwani wengi wanashindwa kutambua kipaji na kujituma katika
soka ni bure kama mchezaji atakuwa na nidhamu mbaya mchezoni.
Hakuna klabu ambayo itakubali kuteketeza kiasi kikubwa cha fedha
kwa kununua mchezaji na kumlipa mshahara kila mwezi huku akiigharimu
kutokana na kuonyeshwa kadi mara kwa mara kwa utovu wa nidhamu.
0 comments:
Post a Comment