Mechi hiyo ambayo hukutanisha bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na
mshindi wa pili wa kinyang'anyiro hicho, itakuwa ya pili kwa miamba hiyo
kukutana ndani ya kipindi cha wiki tatu baada ya timu hizo kuvaana
Julai 30, mwaka huu katika hatua robo fainali ya Kombe la Kagame.
Katika mechi hiyo, Azam ilifanikiwa kutinga nusu fainali baada ya
kuitoa Yanga kwa mikwaju ya penalti 5-3 kufuatia kumaliza dakika 90 bila
kufungana.
Tayari timu zote zipo kambini kujiandaa na mchezo huo wa Jumamosi,
ambao Yanga itahitaji kujituma zaidi ili kulipa kisasi cha kufungwa
Kombe la Kagame, wakati Azam yenyewe itahitaji kuendeleza ushindi wake
dhidi ya wapinzani wao hao.
Azam imeweka kambi visiwani Zanzibar ikiwa chini ya benchi lake la
ufundi linaloongozwa na Muingereza Stewart Hall, wakati Yanga yenyewe
ipo jijini Mbeya ikiwa chini ya Mholanzi Hans van der Pluijm.
Tunatambua ni kawaida katika mechi inayozikutanisha timu hizo
kuwapo kwa vituko na vimbwanga vingi kutoka kwa mashabiki, wapenzi,
wanachama na hata kwa wachezaji, lakini sisi tunatarajia kuona mchezo wa
Kiungwana (Fair Play) ukitawala ili kujenga taswira nzuri ya soka letu
ndani na nje ya nchini.
Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba mashabiki wa Simba huiunga
mkono Azam pale inapocheza dhidi ya watani zao Yanga, jambo ambalo
huongeza ushindani mkubwa kama ilivyo wakati mahasimu hao wa soka nchini
wanapokutana.
Lakini pia tunawakumbusha waamuzi watakaopewa jukumu la kuchezesha
mechi hiyo kutenda haki kwa kufuata sheria zote 17 zinazoongoza mchezo
wa soka duniani, kwani hilo likitendeka litafanya amani kutawala
uwanjani hapo kutoka kwa mashabiki na mwisho dakika 90 kukubali matokeo
kama ilivyo kuwa kuna kushinda, kushindwa na kutoka sare.
Ni wazi mchezo huo utakuwa na ushindani mkali kutokana na timu zote
kufanya maandalizi mazuri huku kila moja ikipania kutwaa ngao hiyo ili
kuukaribisha msimu kwa mafanikio.
Mafanikio Azam iliyoyapata kwa kutwaa Kombe la Kagame na kumaliza
michuano hiyo bila kuruhusu bao ndani ya dakika 90, yanazidisha uwapo wa
upinzani mkali Jumamosi, lakini pia michuano hiyo ilitoa picha halisi
ya idara dhaifu kwa timu hizo ambazo mwakani zitakuwa na jukumu la
kuipererusha bendera ya taifa kwenye michuano ya kimataifa.
Tunaikumbuka vema kauli ya Stewart ambayo aliitoa baada ya
kumalizika kwa michuano ya Kombe la Kagame, kwa kuipongeza safu yake ya
ulinzi kwa kutoruhusu bao ndani ya dakika 90, huku safu ya ushambuliaji
ikifumania nyavu mara 10 kwa muda huo ukiancha yale ya mikwaju ya
penalti.
Ahadi ya Stewart ya kuifanyia kazi safu yake ya ushambuliaji na
kiungo, huku Pluijm naye akikiri kurekebisha kasoro zilizojitokeza
kwenye Kombe la Kagame kabla ya kuivaa Azam, inatufanya kuzidi kuamini
kuwa sheria 17 zikifuatwa Watanzania wataipata burudani waliyoitarajia.
Tunatamani kuona ushindani ukiongezeka zaidi na kufuta ile
dhana ya mechi inayohudhuriwa na mashabiki wengi hapa nchini, ni ya
Yanga dhidi ya Simba tu, lakini hilo litafanikiwa zaidi endapo mchezo wa
kiungwana utatawala viwanjani.
Mwisho wa mchezo, sote tunapaswa kutambua soka ni burudani ambayo
hutuunganisha na kutufanya kusahau tofauti zetu kisiasa, kidini,
kiuchumi na hata kijamii, hivyo hatuna budi kupeana mikono bila kujali
nani kaumizwa na matokeo.
0 comments:
Post a Comment