AWALI nilipokuwa naanza kufuatilia mchezo wa mpira wa miguu mlinda
mlango namba moja alikuwa Mohamed Mwameja na kupewa jina la Tanzania
One.
Nakumbuka kwa miaka hiyo tulikuwa tukibandika picha ya wachezaji na
timu zinazowika kwenye madftari yaliyotumika ili kuonesha mapenzi au
ushabiki.
Katika miaka hiyo ni dhahiri kuwa kwa upande wa walinda mlango jina
la Mwameja lilikuwa juu kutokana na uwezo wake wa kuokoa michomo, kudaka
au kupangua penalti na kupanga walinzi wake vema.
Waswahili wanasema wakati ukuta, baada ya Mwameja kuachana na soka la
ushindani nafasi hiyo ilikaliwa na Juma Kaseja, licha ya umbo lake kuwa
dogo lakini alifanya vema.
Baada ya uwezo wake kufikia tamati kwa sasa naona dhahiri nafasi hiyo
kwa sasa inanyemelewa na mlinda mlango wa Azam FC, Aishi Manula.
Kwa maana uwezo wake unadhihirika katika michezo mingi ya kitaifa na
kimataifa akiwa na kikosi hicho chenye makazi yake Chamazi jijini Dar es
Salaam.
Pia licha ya kufanya vema katika kikosi hicho anafanya vema katika
kikosi cha timu ya taifa ni dhahiri kuwa ikiwa atazingatia maadili
anaweza kufikia kiwango kikubwa na kuwa tegemeo kwa taifa siku zijazo.
Michuano ya Kagame
Nyota huyo katika mashindano ya Kagame ameonesha uwezo mkubwa na
kudhihirisha kuwa ana sifa za kuitwa namba moja Tanzania kwani
ameisaidia kutinga katika hatua ya fainali.
Wakiwa katika hatua ya robo fainali na mchezo wao dhidi ya Yanga alifanikiwa kupangua michomo ya vijana hao wa Jangwani.
Hali hiyo ilifanya kumaliza dakika 90 timu hizo zikiwa sare na
kusababisha kupigiana mikwaju ya penaliti na kufanikiwa kupangua moja
kati ya mikwaju hiyo.
Penalti aliyopangua ilipigwa na Mwinyi Haji, mlinzi aliyesajiliwa na
Yanga akitokea visiwani Zanzibar na kufanikiwa kuiondosha katika
michuano hiyo.
Licha ya hiyo tangu kuanza kwa michuano hiyo hajafungwa bao ndani ya
dakika tisini za mchezo hali ambayo inayoonesha kuwa akiendelea
kuaminiwa ataibeba vema Tanzania.
Baada ya mchezo huo kumalizika, nyota huyo analifafanua kuwa kudaka
penalti kwake ni kitu cha kawaida na ndiyo maana alifanikiwa.
Moja ya maadili anatakiwa kufanya mazoezi ya kutosha, kutoshiriki
anasa, pia anahitajika kufuata ushauri kwa waliomzidi maarifa langoni.
Kipa huyo ambaye ni mwenyeji wa Kilombero mkoani Morogoro tofauti na
kuwa na uwezo mkubwa langoni pia anacheza vema mpira wa wavu.
Hali hiyo inamfanya kuwa na wigo mkubwa wa kuonesha kipaji kingine alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi.
Tofauti na kushiriki michezo, nyota huyo anapenda kusikiliza muziki
wa kizazi kipya na anavutiwa na kila msanii anayefanya ngoma safi.
Nyota huyo pia anaporejea mkoani Morogoro baadhi ya vitu anavyofanya
na kuwa pamoja na rafiki zake wa karibu wakiwemo wachezaji wenzake
aliokuwa akicheza nao kabla ya kufika Ligi Kuu.
Hali hiyo inamfanya kuwa karibu zaidi na wachezaji wenzake sanjari na
kuishi vema na jamii bila kuonesha majivuno au kujisikia kama baadhi ya
wachezaji wanavyofanya baada ya kuonekana wana mafanikio fulani.
Kikubwa kinachotakiwa sasa, mlinda mlango huyo aaminiwe kwa kupewa
dhamana zaidi katika kikosi cha taifa baada ya kufanya vema katika klabu
kwa maana uwezo wake umezidi kuhimalika.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment