Image
Image

Kwa hali hii ya ugonjwa wa kipindupindu kuna haja uongozi uwajibike.

JANA Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadiki amekaririwa akisema idadi ya wagonjwa wa kipindupindu katika mkoa huo imefikia 635 huku akisema umekuwa tishio kwani tayari watu 10 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Akizungumza na waandishi mkoani humo, Sadiki alisema kati ya wagonjwa hao, Wilaya ya Kinondoni inaongoza kwa kuwa na wagonjwa 523. Kutokana na hali hiyo, alipiga marufuku uuzaji wa vyakula shule za sekondari na msingi ili kuzuia ugonjwa huo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema tangu kuanza kwa ugonjwa huo mwezi uliopita kumekuwa na madhara makubwa tofauti na ilivyotarajiwa awali. Ni kweli kabisa kwamba mlipuko wa ugonjwa huo ulipoanza hakuna aliyedhani utaendelea kushika kasi hadi sasa.
Pia, ugonjwa huo umedumu kwa muda mrefu katika mkoa huo tofauti na miaka mingine hali ambayo inazidi kuumiza vichwa vya wengi. Kinachoumiza vichwa ni kwamba hakuna mvua zinazonyesha, lakini ugonjwa huo unazidi kusimika mizizi.
Chanzo kikubwa tunaambiwa ni maji yasiyo salama. Hili nalo ni suala ambalo halikutakiwa kuendelea katika mkoa huo kwa sababu ndipo roho ya nchi ilipo. Kwa msingi huo tuliamini mitandao ya maji ilitakiwa iwe katika mazingira bora tofauti na ilivyo sasa.
Haingiii akilini katika karne hii watu wapoteze maisha kwa kunywa maji machafu. Pia, haiingii akilini ugonjwa kama huo usimike mizizi katika eneo ambalo watu wanaamini kunaishi watu waliostarabika na wenye upeo mpana wa mambo.
Kama Dar es Salaam inakuwa hivyo pembeni mwa nchi hali itakuwaje. Kwa hili tunasema hapana. Ni lazima mtu mmoja mmoja awajibike katika kupiga vita ugonjwa huo. Ni lazima uongozi wa mkoa useme hapana. Ni lazima ukiri kuna tatizo au uzembe mahali.
Haiwezekani eneo ambalo wataalamu wapo kila kona halafu ugonjwa huo uendelee kusambaa. Mungu aepushe mbali tatizo hilo liondoke mapema vinginevyo hali si shwari. Mamlaka husika ni lazima ziwajibike. Tabia ya kufungia maofisini haitamaliza tatizo. Ni lazima watendaji wajipanue.
Ni matarajio yetu uongozi utawajibika inavyotakiwa na kuhakikisha mkoa unakuwa na uhakika wa maji safi na salama. Ni lazima viongozi wahakikishe suala la usafi linatiliwa mkazo, vinginevyo mkoa huu unakwenda kubaya. Mwenye masikio na asikie.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment