WAKATI Waislamu kote duniani wakiwa katika simanzi kuu kutokana na
vifo vya mahujaji zaidi ya 700 katika mji mtakatifu wa Makka, Saudia
Arabia, imethibitika kuwa zaidi ya mahujaji 50 wa Tanzania, hawajulikani
walipo.
Aidha, idadi ya mahujaji wa Tanzania waliokufa katika tukio la
kukanyangana katika mji huo mtakatifu, imefikia watano, baada ya mtu
mmoja zaidi kuthibitika kufa na mwingine kupatikana akiwa majeruhi.
Kutokana na ongezeko hilo la vifo, idadi ya Watanzania waliokufa
wakiwa katika ibada ya Hijja, moja ya nguzo kuu ya Kiislamu, sasa
imefikia watu watano. Hayo yamethibitishwa jana na Mufti wa Tanzania,
Shehe Abubakari Zuberi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari
aliyoituma akiwa Makka.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa “Bakwata kwa kushirikiana na Ubalozi wa
Tanzania Saudi Arabia, tumepata taarifa kwamba maiti mmoja amepatikana,
ametambulika kwa jina la Shafi Khamisi Ali. Pia Nasra Nassor Abdallah
amepatikana akiwa amepata majeraha. Mwenyezi Mungu atawapa tahfif Insha
Allah.
“Kadhalika tumepokea taarifa ya kutopatikana kwa Watanzania 50 ambao
walikuwapo Makka wakati wa tukio hilo. Kati yao 30 walisafiri kupitia
taasisi ya Ahlu Daawa, taasisi ya Khidma watu 17 na TCDO watu watatu.”
Taarifa ya Mufti Zuberi imekuja ikiwa ni mwendelezo wa taarifa juu ya
tukio la kuhuzunisha, lililotokea wiki iliyopita huko Mina, Saudi
Arabia, ambako mahujaji zaidi ya 700 walikufa na wengine kujeruhiwa
wakati wakielekea kwenye Jamaraat, ambapo palitokea msongamano mkubwa.
Alisema anatambua uwepo wa mkanganyiko wa taarifa, ambazo zinazidisha
taharuki kwa ndugu na jamaa wa mahujaji. Hata hivyo, aliwaomba Waislamu
kuwa na moyo wa subira, kwani juhudi za kuwatafuta mahujaji wengine
zinaendelea.
Aliwaombea dua wale waliotangulia mbele ya haki na Mwenyezi Mungu,
apokee ibada zao, awasamehe madhambi yao na awakusanye katika kundi la
waja wema peponi. “Kutokana na mtihani huu kwetu sote, nawaombea dua
wafiwa Mola awape subra na ustahmilivu na kuwaombea wagonjwa wapate
tahfif.
Pia nawaomba Waislamu wote Tanzania kuwaombea dua waathirika wa
mtihani huu. “Mwisho nichukue fursa hii kuwaomba wale wote wenye nafasi
ya kuwafariji na kuwasaidia wanafamilia, ambao katika ajali hii
wameondokewa na nguzo katika familia hizo wafanye hivyo.
Tuwasaidie wanafamilia hawa kwa hali na mali katika wakati huu mzito
sana kwao ili tuwapunguzie majonzi na unyonge walionao,” ilisema taarifa
hiyo ya Mufti. Mufti aliushukuru Ubalozi wa Tanzania nchini Saudia
Arabia.
Alisema wanaendelea kushirikiana na ubalozi huo na vyombo vya
serikali ya Saudi Arabia. Alisema maofisa wa Bakwata waliopo Makka,
wanaendelea kufuatilia habari na taarifa za mahujaji wa Tanzania kwa
umakini mkubwa.
Tukio hilo limetajwa kuwa baya zaidi kutokea wakati wa Hijja katika
kipindi cha miaka 25 iliyopita. Iran imepoteza zaidi ya mahujaji 140.
Idadi ya mahujaji wengine waliokufa na nchi wanazotoka kwenye mabano ni
87 (Morocco), 55 (Misri), 20 (Cameroon), 19 (Niger), 18 (India), 18
(Pakistan), 11 ( Chad), 8 (Somalia), 5 (Senegal).
Nchi za Algeria, Uturuki na Tanzania kila mmoja imepoteza mahujaji
wanne, ingawa jana kiliripotiwa kifo cha mahujaji mwingine wa Tanzania,
hivyo kufanya waliokufa kufikia watano. Nchi za Indonesia, Kenya na
Nigeria kila moja imepoteza mahujaji watatu wakati Uholanzi, Burundi na
Burkina Faso kila mmoja imepoteza mtu mmoja.
Wakati huo huo, taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, jijini Dar es Salaam jana, ilisema idadi ya
watu wa mataifa mbalimbali duniani waliokufa huko Makka, imeongezeka na
kufikia 769 na majeruhi wamefikia 934.
Taarifa hiyo iliyotolewa kupitia Ubalozi wa Tanzania mjini Riyadh,
Saudi Arabia, ilisema tukio hilo la Makka, lilitokea Septemba 24 mwaka
huu na lilitokana na mkanyagano (stampede) wa mahujaji.
“Wizara kupitia Ubalozi huo inaendelea kufuatilia hatma ya mahujaji
wa Tanzania waliopotea katika tukio hilo la ajali ambapo hadi sasa
mahujaji wa Tanzania wapatao 50 bado hawajaonekana.
Vikundi wanavyotoka mahujaji hao na idadi yao ni kama ifuatavyo Ahlu
Daawa- mahujaji 30, Khidma Islamiyamahujaji 16 na TCDO- mahujaji 4,”
ilieleza taarifa hiyo ya Wizara. Vile vile juhudi za Ubalozi wa Tanzania
kwa kushirikiana na Tanzania Hajj Mission na viongozi wa vikundi
vilivyopoteza mahujaji wao, zimefanikiwa kuutambua mwili wa hujaji mmoja
aliyefariki dunia, anayejulikana kwa jina la Shafi Khamis Ali kutoka
kikundi cha Ahlu Daawa.
Kutambuliwa kwa mwili wa hujaji huyo, kunafanya idadi ya mahujaji wa
Tanzania, waliofariki dunia katika tukio hilo kufikia watano. Pia,
Wizara kupitia Ubalozi wake, imepokea taarifa ya kupatikana kwa hujaji
mwingine, anayeitwa Nasra Abdullah akiwa hai, naye kutoka kikundi hicho
cha Ahlu Daawa.
“Mahujaji wengine wa Tanzania wapo salama, ambapo tarehe 26 Septemba
2015 walimaliza Ibada ya Hijja na tarehe 28 Septemba 2015 wameanza
safari ya kurejea nyumbani. Wizara inaendelea kuwaomba wananchi kuwa
watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati serikali ikiendelea
kufuatilia” ilisema taarifa hiyo ya Wizara.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Afya wa Saudi Arabia, Khalid
al-Falih, amekaririwa na mashirika ya kimataifa, akisema kuwa Serikali
ya Saudi Arabia itachunguza vifo vya mahujaji hao zaidi ya 700
vilivyotokea Makka.
Waziri huyo alieleza kuwa uchunguzi utafanyika, kubaini chanzo cha
vifo hivyo, ambavyo havijawahi kutokea kwa zaidi ya miaka 25. “Uchunguzi
utafanyika juu ya tukio la kufa mahujaji katika mji wa Mina.
Tunadhani baadhi ya mahujaji walianza kutembea bila kupata maelekezo
kutoka kwa wahusika maalumu wa kuwaongoza. Uchunguzi utakuwa wa haraka
na tutatoa matokea yake mapema,” alieleza Waziri huyo wa Saudi Arabia.
Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saud Arabia ameagiza uchunguzi
wa kina ufanyike kuhusu tukio hilo na kwamba baada ya kupata matokeo ya
uchunguzi huo, atatoa maamuzi stahiki. Pia, mfalme Salman ameagiza
taratibu za Hijja, ziangaliwe upya.
Awali, ilibainika kuwa mahujaji 717 wamepoteza maisha na wengine 800
walijeruhiwa katika tukio hilo la Makka, wakati watu zaidi ya 2,000,000
walipokuwa wakiswali Ibada ya Hijja. Makundi makubwa mawili ya mahujaji,
yaligongana yalipokutana wakati yakielekea “kumtupia mawe shetani”,
kilometa chache nje ya Makka.
0 comments:
Post a Comment