KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Didas Masaburi, amekiri kukutana
na vijana wanaodaiwa kujifanya wafuasi wa Chadema walioandamana jijini
Dar es Salaam kupongeza hatua ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho,
Dk. Willibrod Slaa, kuacha siasa na kushambulia chama chake.
Juzi vijana hao waliandamana wakiwa na lengo la kwenda makao makuu ya Chadema kabla ya kutawanywa na wananchi.
Tangu asubuhi ya jana, sauti ya Masaburi ilikuwa ikisambazwa kwenye
mitandao ya kijamii akisikika akiwapongeza vijana hao baada ya
maandamano yao kutofikia lengo na baadhi yao kukamatwa na polisi.
Ilipofika mchana, Masaburi aliitisha mkutano na waandishi wa habari
na kukiri kukutana na vijana hao na kuwapongeza kwa kuandamana kwao.
Itakumbukwa kuwa mara baada ya vijana hao kutawanywa juzi, baadhi ya
viongozi wa Chadema Jimbo la Ubungo, walisema maandamano hayo
yaliratibiwa na Masaburi aliyechukua vijana mtaani na kuwavalisha fulana
za chama hicho ili waandamane wakijifanya ni wafuasi wa chama hicho.
Jana, Masaburi alisema hata yeye binafsi angekuwa Chadema angeandamana kuunga mkono hoja zilizotolewa na Dk. Slaa.
“Mimi binafsi niliwaunga mkono vijana baada ya maandamano, lakini
sikuwatuma waandamane. Pia nilisema kuwa vijana wa Chadema wanaorudi CCM
viongozi wote watawaunga mkono.
“Hata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akija CCM nitamuunga mkono na nitamkaribisha vizuri,” alisema Masaburi.
SAUTI YA MASABURI
Sauti hiyo ya Masaburi iliyokuwa ikizunguka kwenye mitandao ya
kijamii, inasikika ikisema: “Vijana waliotokea upande wa Ubungo na
waliotokea Mwenge walikuwa hawaonekani ikaonekana hakuna kilichoendelea
ndio maana mlipata shida.
“Lakini siwakatishi tamaa, ni impact (matokeo) kubwa, hata Kinana,
Magufuli na Rais mwenyewe anajua kinachoendelea, na hakuna vijana
walioongoza vizuri kama Kimara, wameonekana wana uchungu na CCM,
wanahitaji, naomba muendelee na moyo huo, inabidi tuwaandalie vijana wa
Kimara wali pamoja na vijana wengine.
“Hata jana niliwaambia vijana hawa (waratibu wa maandamano hayo)
itakuwaje, aliniambia wapo vijana wengi wa kujitolea na wapo zaidi ya
200 nikajua nitapata hata 20. Vijana 218 idadi hiyo ni kubwa sana,
tunawaomba muendelee na moyo huo huo.”
Sauti ya mmoja wa vijana waliokuwapo ikajibu: “Vijana wengi walijitolea na walikuwa wengi sana, lakini baada ya vurugu kutokea wengi walitawanyika na kuondoka nyumbani.
“Wengi wameondoka nyumbani, na wengine ndio hapo wapo polisi, wapo sita, yaani wengi sana wameondoka wameenda nyumbani.”
Ikasikika tena sauti ya Masaburi: “Wote hao
muwaambie mheshimiwa mbunge mtarajiwa amewashukuru sana, na anasema
lazima tuendelee kushiriki (maandamano), lazima mtaona impact yake na
lazima tuendelee na jitihada hizi kwa sababu tusipofanya hivyo, wale
wanaojiita wana foo wanaweza wakatushinda, hivyo lazima tuwaonyeshe kuwa
nyie ni wezi, mafisadi hata wenzenu wa Chadema hawawataki.
“Ndiyo maana sisi tunaimba hatukutukutu… hatukutaki mnajua huo wimbo?”
Sauti ya vijana ikasikika: “Hatukutaki umepotea na Chama cha Chadema.”
Kisha inasikika sauti ya mmoja wa vijana: “Mimi nilikuwa na wimbo
mpya kidogo ‘Chadema tunahama.. Chadema tunahama…, Slaa kasema kweli…
Slaa kasema kweli.” Akaongeza: “Hii ni hoja mpya iliyokuwepo leo.”
KIjana mwingine: “Hata waandishi wa habari walikuja baada ya watu kukamatwa kamatwa.”
“Walichelewa kidogo,” anasikika kijana mwingine.
Mwingine anadakia: “Hawakuchelewa walikuja wakaondoka.”
Sauti ya kijana mwingine wa kike inasikika: “Yupo
mwandishi wa habari alikuja na gari yake akasimama akasema ninyi mtakuwa
mmetumwa na CCM tukasema hapana, akasema njoo basi tuongee hapa pembeni
tukasema hapana ngoja tuongee ukweli wakasema basi ninyi mtakuwa
mmetumwa. Mara wakasema njoni nyie watatu na viongozi wenu mliokuja nao
tukakataa. Kuna mtu mmoja alikuwa na kadi ya Chadema akaonyesha, dada
mwingine akaja akanisukuma pembeni, akakamatwa, naona ndani kuna wengine
wamewekwa pembeni, naona wengine wanatoka, nikaona hapa hapakaliki.”
Kisha inasikika tena sauti ya Masaburi: “Kosa lingine ambalo
tulilifanya sisi na tumejifunza ni kwamba hatukuweka askari wetu wale
wa kejeli.”
Kijana mwingine anadakia: “Hata sisi tulikuwa na msimamo, tulikuwa
tumejipanga wenyewe, pia tuliwaambia askari wapo, na mwingine akasema
mbona siwaoni askari hapa nikaanza.”
Inasikika sauti ya kijana wa kike: “Wapo watu walikuwa makaburini walikuwa wamejificha.”
Kisha inasikika tena sauti ya Masaburi: “Pale
makaburini walikuwepo watu karibu na magari, wale ni fundi magari
wanatengeneza karibu na makaburi, lakini ni wanachama wa Chadema.”
Anasikika kijana mwingine: “Yaaani safari nyingine
tunatakiwa tuwe na kadi za Chadema, wakati tupo kule ndani tuliulizwa
kadi ziko wapi kwa sababu tungekuwa nazo aaaaaa, una kadi ya CCM halafu
unahojiwa unashindwa kujieleza.
“Tungekuwa na kadi tungeweza kujieleza. Kijana mmoja aliingia
akajitoa muhanga nikamwambia aangalie hakuna mtu wetu aliyebaki huko
wakati tunawasiliana na wewe, mimi polisi si tatizo, tatizo langu ni
kubaki mle ndani, anaweza akamnyonga mtu. Mimi najulikana sana mle
ndani.”
Akasikika tena Masaburi: “Mimi nimemwambia
mheshimiwa nije niwasalimu na zawadi yangu kubwa ninayoweza kuwapa ni
kuwashukuruni na kuwatia moyo tuendelee na moyo huo huo ndio CCM
itakuwa chama.
“Maana yake wale wanafanya mambo kama haya haya wanaandamana hivi,
unaonaje tena kwa nguvu zote wakiimba kwa nguvu zote na kuruka ruka
Lowassa… Lowassa…. na sisi CCM tusipofanya hivyo hatuwezi kwenda mbali,
lazima na sisi tuamke tujibadilishe wenyewe ili tuweze kuendeleza chama
chetu.
“Mimi sina mengi zaidi ya haya, lengo langu ni kuwasalimu,
kuwashukuru na kuwaambia watu tupo pamoja na kupata majina ili tuweze
kuwajua.”
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment