Hali ya mkanganyiko katika mkutano huo wa Lowassa, anayeungwa pia
na muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya
NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), ilianza kuonekana mapema
wakati maelfu ya watu walipojitokeza kwenye viwanja vya Tangamano.
Baadhi ya watu, hasa wanawake walijikuta wakiwa hoi hoi kutokana na joto
na kukosa hewa, hali iliyowalazimu wahudumu wa Msalaba Mwekundu
kuingilia kati na kutoa huduma ya kwanza kwani wengi wao walionekana
wakizimia na kuanguka chini.
“Asanteni sana kwa mapokezi yenu. Hali iliyopo sasa sio
nzuri…asanteni tena kwa mapokezi mazuri," alisema Lowassa kabla ya
kuomba kura na kutaka mkutano huo usitishwe kwa kuhofia usalama wa watu
kwenye uwanja huo ulioonekana kuwa mdogo.
“Katika hali hii, niseme tu nimefika kuwaombeni kura,” alisema
Lowassa, kabla Meneja wa kampeni, John Mrema hajapanda jukwaani na
kutangaza kuahirisha mkutano huo hadi siku nyingine kwa kuhofia kuwa
msongamano huo ungeweza kusababisha vifo.
“Tunalazimika kuahirisha mkutano huu wa mgombea urais kwa hofu ya
watu kufariki,” alisema Mrema na kuwaomba wananchi hao kuondoka.
Hata hivyo, umati wa watu uligomea tangazo hilo, ukimtaka Lowassa kuendelea kuzungumza nao.
Tangazo la kuahirishwa kwa mkutano huo lilikuja muda mfupi baada ya
Lowassa kukaribishwa na Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ili
azungumze na wananchi.
Hali hiyo iliufanya uongozi wa kampeni uliokuwapo kuamua kutengua
uamuzi wao wa awali wa kusitisha mkutano huo na kumruhusu Lowassa
kuzungumza na wananchi.
Aliposimama, Lowassa aliwasalimu kwa salamu ya People’s na wao
wakajibu kwa sauti kubwa Power. Akizungumza na wananchi hao kwa mara ya
pili, Lowassa alisema akichaguliwa atafufua Bandari ya Tanga, atafufua
reli,
kufufua viwanda na kuboresha kilimo.
Hata hivyo, wananchi walisikika wakimtaka azungumzie suala la
mwanamuziki Babu Seya, naye akasema akichaguliwa kuwa rais,
atalishughulikia suala hilo kwa mujibu wa sheria.
Sumaye alipopata nafasi ya kuzungumza, aliwashukuru wana Tanga kwa
kuhudhuria kwa wingi mkutano huo, huku akiwapa pole kwa msongamano
mkubwa uliokuwepo.
Aliwaomba watu waliokuwa sehemu mbalimbali uwanjani hapo kukaa
chini na wale ambao walikosa hewa wasaidiwe mara moja, hasa wanawake na
watoto
MABOMU YARINDIMA
Baada ya mkutano kumalizika, baadhi ya wananchi waliohudhuria
mkutano huo walijikuta wakivurumishiwa mabomu ya machozi na polisi baada
ya kuonekana wakiandamana huku wengine wakikimbia mchakamchaka na
kupita jirani na ofisi ya CCM katika Barabara ya 20 jijini hapa. Mtaani
hapo, pia kuna ofisi ya CUF ambayo ina ngome yake ya kutumainiwa jijini
hapa.
Makundi ya wananchi hao, hasa vijana walikuwa wakiimba nyimbo
mbalimbali za kumsifia Lowassa kuiponda CCM, hali iliyozua hofu kuwa
pengine panaweza kuibuka mtafaruku kwa kufanya vurugu katika ofisi za
CCM.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi jijini Tanga hakupatikana jana kuzungumzia hali hiyo kiundani.
LOWASSA ATAKA SIKU 100
Awali, akiwa katika Jimbo la Bumbuli, Lowassa alisema anahitaji
siku 100 tu za kuwa Ikulu baada ya kuapishwa ili amalize kero kuhusia na
ukosefu wa dawa hospitalini, madai ya walimu na pia kumaliza matatizo
ya watumishi wote wa umma yanayohusiana na maslahi yao.
Alisema ana uhakika wa kushughulikia matatizo hayo ndani ya siku
chache baada ya kushinda uchaguzi mkuu Oktoba 25 na kuapishwa kwa vile
matatizo hayo anayajua vizuri na hivyo hakuna sababu ya kuchelewa katika
kuyapatia ufumbuzi.
"Matatizo ya walimu na watumishi wengine nayajua... jitokezeni kwa wingi siku ya kupiga kura na kuleta mabadiliko," alisema.
Alisema kuweka dawa katika zahanati na hospitali hizo kutaenda sambamba na uwepo wa wataalamu mbalimbali.
Kadhalika, Lowassa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu katika awamu ya
kwanza ya Rais Jakaya Kikwete, alisema matatizo ya ukosefu wa dawa
katika zahanati, vituo vya vya na hospitali za umma yatafikia ukomo
ndani ya siku hizo 100 atakazokuwa madarakani kwani eneo hilo ni
miongoni mwa vipaumbele vyake vikubwa pindi akichaguliwa na kuwa rais wa
awamu ya tano.
Pia, Lowassa aliahidi kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu
baina ya wananchi wanaojihusisha na kilimo cha chai Bumbuli na
wawekezaji, Kiwanda cha Chai cha Mponde kinachodaiwa kufungwa kwa sababu
za kisiasa, akisema kuwa tatizo hilo litabaki kuwa historia ndani ya
miezi sita ya kuwa kwake madarakani.
"Tumechoka... amekuja Mkuu wa Mkoa, amekuja Rais, amekuja Makamba, hakuna kilichofanyika.
Nawahakikishia nitamaliza tatizo hili," alisema Lowassa na kuongeza:
"Nitahakikisha tatizo hili linapata ufumbuzi, wakulima wanauza chai
yao na kiwanda kinafanya kazi," alisema Lowassa na kuibua shangwe
kubwa.
Katika hatua nyingine, Lowassa aliwataka wananchi wa Bumbuli
kutofanya makosa kwa kumchagua tena mbunge anayetetea nafasi yake
jimboni humo, January Makamba, kwa kudai kuwa yeye (Makamba) na Chama
Cha Mapinduzi (CCM) hawana tena uwezo wa kushughulikia kero zao.
Aliongeza kuwa mabadiliko ya kweli kwa Watanzania yatapatikana kwa
kuiondoa CCM madarakani na hivyo akamshauri Makamba kuihama CCM na kutua
Ukawa kwani yeye bado ni kijana na hivyo hana sababu kubaki katika
chama ambacho mwisho wake wa kuongoza nchi utafikiwa baada ya uchaguzi
Oktoba 25.
Lowassa aliendelea kuahidi kuanzisha benki maalumu kwa ajili ya
mama lishe na waendesha bodaboda kuweza kupata mikopo mbalimbali kwa
ajili ya kujikwamua na umaskini.
“Serikali yangu nitaiongoza kwa ‘speed’ 120, itakuwa ya vitendo
zaidi badala ya longolongo, magoigoi wote watabaki CCM,” alisema.
Aidha, alirejelea kauli yake ya siku zote kuwa anauchukia umaskini
na amechoshwa kusikia kero za michango ya shule, dawa na huduma duni za
matibabu na kwamba ndani ya miaka mitano Tanzania itabadilika.
0 comments:
Post a Comment