Muamuzi Ruddy Buquet jana alilazimika kusimamisha mchezo wa
ligi daraja la kwanza nchini Ufaransa kati ya Olympic Marseille dhidi ya
Olympic Lyon, baada ya mashabiki wa timu mwenyeji kuanzisha fujo katika dakika
ya 62.
Mashabiki wa Olympic Marseille walianzisha zogo kwa kurusha
chupa, mafataki pamoja na mabaki ya vyakula sehemu ya kucheleza hali ambayo
ilileta taharuki kwa wachezaji pamoja na mashabiki wa timu pinzani.
Kutokana na hali hiyo muamuzi alilazimika kupuliza kipyenga
cha kusimamisha mchezo na kuwaamuru wachezaji waingie katika vyumba vya
kubadilishia kwa usalama.
Askari wa kutuliza ghasia katika uwanja wa Velodrome
walilazimika kuingia uwanjani wakia na vifaa vya kazi na kuanza kutuliza ghasia
ambazo zilikua zinaendelea kutanda miongoni mwa mashabiki wa timu mwenyeji
kwenda kwa wenzao wageni.
Sababu kubwa ya balaa hilo kutokea uwanjani hapo, limetajwa
kuwa ni hasira za mashabiki wa Olympic Marseille kumuona aliyekua mchezaji wao
Mathieu Valbuena, akirejea uwanjani hapo akiwa na timu pinzani.
Hata hivyo mchezaji huyo alionesha kuwapuuza mashabiki na
aliendelea kucheza soka japo alikua akipata wakati mgumu alipokua akicheza
sehemu za pembeni mwa uwanja na kupiga mipira ya kona.
Pamoja na mambo hayo kujitokeza, hali ilirejea kuwa shwari
na muamuzi Ruddy Buquet alizirejesha timu uwanjani na kumalizia mchezo ambao
ulishuhudia timu hizo mbili zikifungana bao moja kwa moja.
Mathieu Valbuena aliihama Olympic Marseille mwaka 2014 baada
ya fainali za kombe la dunia na kutimkia nchini Urusi baada ya kusajili na
klabu ya Dynamo Moscow, lakini mwanzoni mwa msimu huu alirejea nchini Ufaransa
na kusajiliwa na Olympic Lyon.
Mathieu Valbuena alikua mchezaji wa Olympic Marseille tangu
mwaka 2006 na aliitumikia klabu hiyo katika michezo 242 na kufunga mabao 27.
0 comments:
Post a Comment