Aidha, serikali imewasisitizia wananchi kutumia vizuri mitandao
kwa faida yao na taifa na kujiepusha na mambo ambayo yanakatazwa na
sheria hiyo ili kutoingia matatani.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
Prof. Makame Mbarawa, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam jana kuhusu kuanza rasmi kutumika kwa sheria hiyo na ya
miamala ya kielektroniki.
“Serikali imejiridhisha baada ya kufanya maandalizi yote muhimu
ikiwamo kutoa elimu kwa umma na kujenga uelewa kwa watekeleza wa sheria
hizi. Sasa sheria hizi zitaanza kutumika rasmi Septemba 1 (leo),”
alisema Prof. Mbarawa.
Alisema sheria hiyo itasaidia kupambana na uhalifu kwenye mtandao
kutokana na watu wengi kutumia vibaya mtandao na kuwalaghai watu kutuma
fedha ama kuiba katika mabenki.
Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, watu wanaosambaza meseji za
uchochezi ama za uongo kwa watu wengine ni kosa la kisheria na kufanya
hivyo watakumbana na adhabu kali.
Alisema mtumiwaji wa meseji za aina hiyo akifuta pasipo kusambaza kwa watu wengine sheria hiyo haitamwadhibu wala kumhusu.
“Sehemu ya kifungu cha sheria ya makosa ya mtandao, kifungu cha 16
kinaeleza: mtu atakayechapisha taarifa au data katika picha,
maandishi, alama au katika namna nyingine yoyote katika mfumo wa
kompyuta, huku akijua kwamba taarifa au data hizo ni za uongo,
zinapotosha, zisizo sahihi, na kwa lengo la kudhalilisha, kutishia,
kuudhi au kwa njia nyingine au kudanganya umma au kuchochea utendaji wa
kosa, atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atalipa faini
isiyopungua Sh. milioni tano au kutumika kifungo kisichopungua miaka
mitatu au vyote kwa pamoja,” alisema.
Prof. Mbarawa alitoa wito kwa wananchi wazingatie matumizi salama
na sahihi ya huduma za mawasiliano na mitandao kwa manufaa ya kila mtu
na kwa maendeleo ya taifa na kuepuka matumizi yasiyo sahihi.
0 comments:
Post a Comment