NCHI
yetu sasa hivi iko katika kipindi cha kampeni, ambazo zitatusaidia
kuingia kwenye chumba cha kupigia kura Oktoba 25 mwaka huu tukiwa na
uelewa mpana ni kwa nini tunamchagua fulani na siyo fulani.
Ni uchaguzi utakaotupatia viongozi, watakaotuongoza kwa kipindi
kingine cha miaka mitano.
Kwa mantiki hiyo,hiki ni kipindi muhimu sana
kwani hawa wanaonadi sera zao sasa ili tuwachague kwa nafasi mbalimbali
za urais, wabunge, wawakilishi, madiwani na masheha, ama watatupeleka
kwenye ‘nchi ya maziwa na asali’ au watatupeleka pabaya.
Kwa lugha nyingine,ni sisi wapiga kura ambao tuna ‘rungu’ la
kupitisha ni nani hasa watuongoze kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Ni kwa sababu hiyo, ni lazima, kwa kila aliyejiandikisha, kujua kwamba
ana dhima kubwa na muhimu ya kuchagua kiongozi ambaye amempima na
kugundua kwamba ana uwezo wa kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu.
Je, tutawajuaje hawa wagombea kwa sura na sera zao? Je, kweli
tutakapokuwa tunaelekea kwenye sanduku la kura, tutakuwa na uhakika
kwamba tunafanya uchaguzi sahihi? Ili kufikia uamuzi mzuri ni muhimu
tuwafahamu vyema wagombea hawa na jambo moja la kufanya ni kuhudhuria
kwenye mikutano yao ya kampeni ili kuwasikiliza.
Lakini, mbali na mikutano ya kampeni, moja ya vitu vinavyotumiwa na
wagombea kujinadi katika kampeni hizi na sisi kuzidi kuwafahamu hata kwa
sura wagombea wetu ni mabango.
Mabango haya hubeba picha za wagombea, kuanzia wa urais, ubunge,
uwakilishi hadi udiwani na mengine huwa pia na ujumbe mfupi, unaoonesha
mtazamo wa mgombea husika katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Mbali na mabango, wagombea pia wanaruhusiwa katika kipindi hiki cha
kampeni kugawa vipeperushi, kuchapisha fulana na kofia, kutoa vipindi
katika vituo vya runinga na redio na hata kuandika makala kwenye
magazeti ili kueleza yale wanayoyaamini.
Aghalabu njia hizi za kampeni zina manufaa kwa pande zote mbili; kwa
wapiga kura kuwaelewa wagombea wao hadi kwa sura kama watashindwa
kutembelea kampeni zao na kwa wagombea nao kutufikishia zaidi kile
walicho nacho. Na njia hizi mbalimbali zinazotumiwa na wagombea katika
kutufikia zinawagharimu pesa nyingi.
Lakini sasa hivi ukipita katika baadhi ya mitaa, utakuta mabango
mengi ya wagombea yakiwa yamechanwa, yamechorwa, yameandikwa maneno ya
kebehi au yakiwa yametobolewa macho, masikio au midomo.
Kinachojitokeza ni kwamba asilimia kubwa ya mabango haya, yanachanwa
kwa hujuma, kwani unaweza kukuta sehemu lilikobandikwa bango la mgombea
wa chama fulani, limechanwa na kubandikwa la mgombea wa chama kingine.
Au unaweza kukuta bango la mgombea lililobandikwa juzi tu, limechanwa
katika eneo ambalo mabango ya muda mrefu yasiyohusu uchaguzi, yapo.
Kitendo hiki mbali na kuvunja sheria za nchi, si cha kiungwana abadani
na hakina tija hata kwa huyo anayechana.
Ni kitendo kinachoweza kusababisha uvunjifu wa amani, pale aliyeweka
bango lake au wafuasi wake, watakapomkuta mtu akichana au watagundua
kwamba limechanwa na fulani. Ni vyema wananchi tukaacha hii tabia kwa
sababu hatuna sababu ya kugombana na mabango, bali tushindane kwa hoja.
0 comments:
Post a Comment