Jeshi la Polisi nchini limetangaza kuanza kutumika nchini kwa kanuni mpya za tozo la papo kwa papo kwa njia ya kieletroniki.
Pia jeshi hilo litaanza utaratibu wa kuweka nukta katika leseni za madereva watakaopatikana na makosa mbalimbali.
Kanuni ya kutoza tozo la papo kwa papo imo kwenye Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 iliyorejewa mwaka 2002.
Jeshi la Polisi limesema kuwa kanuni hiyo itatumika kulipisha faini za papo kwa hapo kwa njia ya mtandao.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuongezeka kwa malalamiko kutoka kwa wamiliki wa magari na madereva wakidai wamekuwa wakilipishwa faini bila ya kupewa risiti halali za serikali (GRR).
Mfumo huu ulianza kutumika kuanzia jana kwa majaribio katika Jiji la Dar es Salaam ili kubaini changamoto zitakazojitokeza kwenye mfumo huo.
Chini ya utaratibu huu mpya, watu watakaopatikana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani, watatakiwa kulipa faini zao kwa njia ya mitandao ya simu au kwenye mashine za kutolea fedha (ATM).
Pia kuna kanuni ya kuweka pointi kwenye leseni kwa madereva ambao watakaopatikana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani.
Tunalipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua hii kwani tunaamini kwamba itasaidia kwa kiasi kikubwa serikali kukusanya mapato.
Kimsingi, yamekuwapo malalamiko ya muda mrefu juu ya askari wachache kutokuwa waaminifu kwenye zoezi la kutoza faini na kutoa risiti kwa wanaopatikana na makosa ya usalama barabarani.
Zipo taarifa kwamba kipo kikundi kidogo cha askari wa usalama barabarani wasiokuwa waaminifu ambao wamefikia hatua ya kutengeneza vitabu bandia vya risiti kwa ajili ya kukusanya fedha kwa njia isiyo halali kutoka kwa wavunja sheria za barabarani.
Lakini kwa uamuzi huu, sisi tuna matumaini makubwa kwamba utakuwa na tija katika suala zima la kukusanya faini.
Aidha, adhabu hizi zinatakiwa kuwa msaada kwa taifa katika kukabiliana na madereva wazembe na kupunguza ajali nchini ambazo zimesababisha nguvu kazi ya taifa kupotea.
Ni wazi kwamba Tanzania imekuwa na tatizo sugu la ajali nyingi ambazo kwa sehemu kubwa huchangiwa na uzembe wa madereva.
Hata hivyo, kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko juu ya udhibiti wa matatizo ya uzembe wa madereva barabarani.
Hali hiyo ilichangiwa zaidi na baadhi ya askari wa usalama barabarani kutuhumiwa kupokea rushwa na kuwaachia madereva wazembe.
Na hata ilipoanzisha utaratibu wa faini, bado baadhi ya wajanja wachache wanadaiwa kutengeneza vitabu na kutoa risiti feki na kuzitafuna fedha za serikali.
Hata hivyo, pamoja na juhudi hizi za serikali kubuni utaratibu huu mpya wa ulipaji faini kwa njia ya kielektroniki, tunatahadharisha kuwa usigeuke na kuwa mwanya mwingine wa kuongeza ulaji wa rushwa.
Hii inawezekana kwa kuwa baadhi ya madereva watakaotozwa faini, watashawishiwa askari wasio waaminifu watoe rushwa na kuachiwa na hivyo kuikosesha serikali mapato.
Tunatoa wito kwa wananchi kuheshimu kanuni hizi na kulipa faini kwa utaratibu halali badala ya kutoa rushwa ambayo itawanufaisha askari wachache wasiokuwa waaminifu huku serikali ikikosa mapato.
0 comments:
Post a Comment