Image
Image

Wanawake wa Tanzania wana maslahi maalum na uchaguzi mwaka huu – Rais Kikwete.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa wanawake wa Tanzania wana maslahi maalum na Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa sababu kwa mara ya kwanza wanawake wanaweza kutoa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa wanawake wa Tanzania wana maslahi makubwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa sababu safari ya Tanzania kupata Rais mwanamke imeanza nchini kwa chama kimoja cha siasa kuteua Mgombea Mwenza mwanamke.

Rais Kikwete pia amesema kuwa wanawake wa Tanzania wanastahili kuwa na maslahi yasiyokuwa ya kawaida katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa sababu uchaguzi huo unaweza kuamua kama Tanzania inaendelea kuwa ya amani na utulivu ama inaingia katika machafuko kulingana na matokeo ya uchaguzi huo na kuwa hali ya machafuko, kama ilivyo pote duniani, itawaathiri zaidi wanawake na watoto.

Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alikuwa anazungumza na makatibu wa mikoa na wilaya wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) usiku wa Jumapili, Septemba 6, 2015, katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Usambara Safari Lodge ya Morogoro. Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na Mgombea Urais wa CCM mwaka huu, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli.

Kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, 2015, uliopangwa kufanyika Oktoba 25,  CCM kimemteua Mheshimiwa Samia Hassan Sululu kuwa Mgombea Mwenza kwenye tiketi ya Chama hicho ikiwa ni mara ya kwanza kwa chama hicho tawala na kikongwe kumweka mwanamke kwenye tiketi yake ya urais katika historia ya Tanzania.

Rais Kikwete ambaye aliwasili Morogoro asubuhi kwa ajili ya kuhutubia mkutano huo amesema kuwa wanawake wote wa Tanzania, bila kujali, itikadi zao za kisiasa wanastahili kuwa na maslahi maalum na Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa sababu kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania wanawake wanaweza kupata Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Tanzania mwanamke.

“Nyie kinamama wa CCM, na kwa hakika wanawake wote wa Tanzania, mnastahili kuwa na maslahi maalum na Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa sababu katika historia ya nchi yetu, nchi hii ya Tanzania inaweza kupata Makamu wa Rais mwanamke. Imekuwa safari ndefu na yenye changamoto nyingi ,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Kuteuliwa kwa Samia Sululu Hassan ni ishara kuwa safari ya Tanzania kuwa na Rais mwanamke imeiva – iwezesheni safari hiyo ifanikiwe katika nchi yetu nyie akinamama. Na wala uteuzi wa Samia haukuwa wa bahati mbaya. Mgombea Urais wa CCM, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli alitaka mwanamke awe ndiye mgombea mwenza.”   

Rais Kikwete amesema kuwa uteuzi wa Samia hakuwa wa bahati mbaya kwa sababu tokea mwanzo CCM ilitaka kuwa na Mgombea Mwenza mwanamke. Hivyo, hakuna jina la mwanaume lililojadiliwa katika vikao vya uteuzi.

“Huu ulikuwa mwendelezo wa sera zetu kwa akinamama. Mtakumbuka kuwa kwa mara ya kwanza katika mchakato wetu wa kutafuta Mgombea Urais, akinamama wawili waliingia katika tano bora kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu na wawili hatimaye wakaingia katika tatu bora kwenye Mkutano Mkuu kabla ya kuteuliwa Mheshimiwa Magufuli,” amesema Rais Kikwete na kusisitiza:

“Hata kwenye Katiba Inayopendekezwa, CCM ilipigia na imepata asilimia 50-50 ndani ya Bunge kati ya wanawake na wanaume. Haya mnayoyaona siyo ya bahati mbaya hata kidogo. Ni sera za makusudi za kumwinua mwanamke wa Tanzania.”

Kuhusu hali ya baadaye ya Tanzania baada ya uchaguzi, Rais Kikwete amesema kuwa lugha za vyama vinavyowania kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu huo zinaonyesha kuwa wanawake wa Tanzania lazima wachague kati ya amani na utulivu ama machafuko na umwagaji damu.

“Mnasikia wenyewe, sisi siku zote tunahubiri amani na utulivu kama msingi mkuu wa maendeleo ya nchi yetu….wenzetu wale wanahubiri habari ya nchi hii itamwaga damu…wanajiandaa kumwaga damu ya Watanzania…lakini kama nilivyopata kusema huko nyuma huu ni moto wa mabua. Mwanzoni walidhani kuwa nchi haina wenyewe….nadhani sasa wameanza kugundua kuwa nchi hii ina wenyewe…nyie wananchi wa Tanzania.”
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment