Rais JAKAYA KIKWETE ameweka jiwe la msingi na kuzindua rasmi mradi wa uchimbaji wa madini ya Urani katika Mto Mkuju, Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma.
Mradi huo unatarajia kuliingizia taifa mapato ya zaidi ya Dola Milioni 968 kwa kipindi cha miaka kumi ya uzalishaji.
Rais KIKWETE pamoja na kuitaka kampuni hiyo kuzingatia masuala ya usalama yanayotokana na athari ya madini hayo, pia amesema mradi huo una manufaa makubwa mno katika maendeleo ya taifa, hasa katika sekta ya kuliingizia taifa mapato na ajira kwa Watanzania.
Kwa miaka zaidi ya saba, kampuni ya Mantra Tanzania, imekuwa ikifanya utafiti wa madini ya Urani katika eneo hilo la Mto Mkuju.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, FREDRICK KIMBODIA amesema wanatarajia kuchimba madini hayo tani Elfu-70 kwa muda wa miaka 10 na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya 10 Duniani itakayokuwa inachimba madini ya Urani.
Rais KIKWETE alipokuwa njiani kwenda kwenye eneo la mradi huo, wananchi wa kijiji cha Likuyu Sekamaganga, kilichopo jirani na mradi huo walisimamisha msafara wake na kumueleza kero mbalimbali ikiwemo ya kuitaka kampuni ya Mantra pindi uchimbaji utakapoanza kujenga makazi ya wafanyakazi katika kijiji hicho ili wanufaike na kukua kwa mji.
0 comments:
Post a Comment