JOPO la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo
linatarajia kuanza kusikiliza kesi ya kikatiba kuhusu haki ya mpigakura
kukaa umbali wa mita 200 kama ni sahihi au la.
Jopo hilo la majaji Seleman Kihiyo, Aliyisius Mujuluzi na Lugano
Mwandambo, liliteuliwa baada ya mgombea ubunge wa Viti Maalumu Jimbo la
Kilombero kupitia Chadema, Amy Kibatala, kufungua kesi hiyo kupitia kwa
wakili Peter Kibatala.
Katika maombi yake, anaomba Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es
Salaam itoe tafsiri sahihi ya kifungu cha 104 (1) cha sheria ya
uchaguzi kuhusu haki ya mpigakura.
Mdai anaiomba mahakama hiyo iseme kwa mujibu wa kifungu hicho,
wananchi baada ya kupiga kura wanaruhusiwa kukaa kwa utulivu umbali wa
mita 200 au la.
Wakili Kibatala, alifungua kesi hiyo chini ya hati ya dharura katika
Masjala Kuu ya Mahakama Kuu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Amy aliyejitambulisha kama mpigakura mwenye masilahi na uchaguzi,
anaiomba mahakama itoe tafsiri ya kifungu hicho sura ya 343 iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2010.
Anaiomba mahakama itafsiri kuhusu haki hiyo kwa wananchi, kwamba ni
sahihi kwa wale wasiofanya kampeni kukaa umbali wa mita hizo au la.
Pia, anaiomba mahakama iiamuru NEC kutamka kwamba huo ni uvunjifu wa
kikatiba kwa kuwazuia na kuwatishia wananchi kwamba watakiona cha moto.
Kifungu cha 104 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343
kinasema: “Hakuna mtu atakayefanya mkutano siku ya kupiga kura katika au
ndani ya jengo lolote ambamo upigaji kura katika uchaguzi unaendelea,
au mahali popote ndani ya eneo la mita 200 ya jengo hilo, kuvaa au
kuonyesha kadi ya picha yoyote, upendeleo au nembo nyingine inayoonyesha
kuunga mkono mgombea fulani katika uchaguzi.”
0 comments:
Post a Comment