Image
Image

Kifo cha Mtikila utata mtupu.

UONGOZI wa juu wa Chama cha Demokratic (DP), umesema kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho,Christopher Mtikila, kina utata na kulitaka Jeshi la Polisi na vyombo husika kuchunguza.
Kimesema chama hicho kinashangazwa na kimeshtushwa na kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo chake kwani, kimetokea katika kipindi kigumu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwa niaba ya chama, Naibu Katibu Mkuu DP Bara, Abdul Mluya, alisema chama hicho kimepokea msiba huo kwa mshtuko na masikitiko makubwa.
Alisema mbali na mazingira ya ajali hiyo, lakini kumekuwa na picha mbalimbali za ajali zinarushwa kwenye mitandao ya kijamii, bado imekuwa kitendawili kwao.
“Kifo cha mwenyekiti na mpiganaji wetu kimetushtua kwani, hata kwenye picha za kwenye mitandao ya kijamii zimekuwa zikionekana kama tayari alifanyiwa huduma ya kwanza, jambo ambalo si la kweli.
“Kiukweli hizi picha hazitufurahishi kwani, inatutia mashaka kwamba, mpigapicha wa picha hizi alikuwa wapi, kulingana na hali ya mazingira ya ajali haikuwa rahisi kwa watu kufanya hivi. Hii inaonekana dhahiri ajali hii imetengenezwa,” alisema.
Alisema kifo hicho kinawatia mashaka kutokana na mara kwa mara marehemu kufuatiliwa kwa ukaribu na watu wasiofahamika kwa nyakati tofauti tofauti.
Mluya alisema marehemu kabla ya kupata ajali, Septemba 25 na 26 wakiwa katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara, waliingiwa na wasiwasi baada ya kuona baadhi ya watu wakiwafuatilia.
“Baada ya kufuatiliwa kwa hali isiyo ya kawaida, nilimshauri mwenyekiti kuhama hoteli hiyo na kuelekea mkoani Mwanza,” alisema.
Alieleza kuwa, wakati wakiwa njiani kuelekea Mwanza, katika eneo la Serengeti gari lisilofahamika lilikuwa likiwafuatilia, jambo ambalo lilimtia mashaka marehemu hivyo, kuamua kumpa taarifa katibu huyo.
Alisema kuwa, kulingana na kufuatiliwa huko na hali ya mienendo na misukosuko ya kampeni zinazoendelea, marehemu aliandaa press (mkutano wa waandishi wa habari), ambayo iliwagusa baadhi ya wanasiasa nchini, hali hiyo ni miongoni mwa mambo yanayowatia mashaka.
Katibu Mkuu huyo alisema pamoja mambo hayo, chama hicho kitaendelea kusimamia misingi na yale mazuri yaliyofanyika wakati wa uhai wake katika harakati zake za kupigania ukombozi wa Watanzania.
“DP itaendelea kumuenzi na yale ambayo alitamani kuyaona wakati wa uhai wake kwa kuhakikisha tunayafikia. Shughuli za kichama katika kampeni zitaendelea katika kuhakikisha tunafanikiwa,” alisema.
Kaimu Mwenyekiti.
Akizungumzia kifo hicho, Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Peter Maguira, alisema chama hicho kimeshtushwa kupokea msiba huo kwani kimetokea katika kipindi kigumu kwani, alikuwa dira ya chama hicho.
“Mchungaji Mtikila alikuwa dira ya chama hivyo kifo cghake kimetuumiza sana kwani mazingira ya kifo hicho yamewaacha njia panda,” alisema.
Hivyo, Makamu mwenyekiti huyo ambaye kwa sasa anakaimu nafasi ya mwenyekiti kwa muda, aliiomba Serikali kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kufanya uchunguzi kuhusiana na kifo hicho.
Hali ilivyokuwa awali.
Kwa upande wake, Mchungaji Patrick Mgaya, aliyejitambulisha kama msaidizi na ndugu wa karibu wa marehemu Mtikila, alisema kuwa, wakati marehemu akiwa katika harakati zake za kampeni, alikuwa akifuatiliwa kwa hali isiyo kawaida, jambo ambalo liliwatia mashaka katika kipindi hicho.
“Wakati marehemu akiwa katika mkutano wa kampeni mkoani Njombe, zilipita pikipiki zilizokuwa na bendera mbili za vyama viwili tofauti zilipita mbele ya Mchungaji Mtikila, nilipojaribu kumziba, ghafla zilipotea na kutokomea,” alisema.
Alisema baada ya kumaliza mkutano huo, Oktoba 4, mwaka huu, wakiwa njiani kutoka Njombe kurudi Dar es Salaam kulikuwa na gari aina ya Toyota Land Cruser ya kijivu iliyokuwa ikiwafuatilia, jambo ambalo marehemu alionesha wasiwasi na kumtaka dereva apunguze mwendo ili kulipisha lipite.
Hata hivyo, alisema katika mazingira ya kushangaza, walipoanza kuondoka baada ya kulipishal waliliona gari hilo, ambapo dereva wa gari lao alijaribu kulipita. lakini kila alipojaribu kuongeza mwendo, gari hilo liliongeza mwendo na kuwafuatilia.
Alieleza kuwa, walipofika eneo la Mikumi mkoani Morogoro, marehemu alihitaji kuchimba dawa, ambapo walitumia nusu saa kwa ajili ya kulipisha gari hilo liondoke. Lakini baada ya kufika mkoani Morogoro, gari hilo lilionekana kuwafuatilia.
Alisema wakiwa katika mwendo wa kasi huku wakifukuzana na gari hilo, walipofika eneo la Mdaula, ambapo ajali ilipotokea walikutana na lori lililokuwa limepaki, ghafla lilitokea lori lingine kwa gari hilo ambalo hawakupata namba zake, lilipita kwa hali isiyo ya kawaida na ghafla lori hilo liliwafuata na kutaka kuwagonga.
Aliongeza kuwa, baada ya roli hilo kuwafuata, dereva wao alijaribu kukwepa huku wakiwa katika mwendo kasi, hatimaye lilikwenda mita 150 kutoka eneo la barabara (kwa mujibu wa jeshi la polisi), na kutumbukia kwenye shimo.
“Baada ya gari kupinduka, nilibaki kwenye gari na hakukuwa na mtu mwingine, nilipoanza kuita ghafla nilimsikia dereva akidai kapotelewa na simu yake hivyo, anaitafuta badala ya kutafuta wenzetu ambao hatukuwaona,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, wanaitilia shaka ajali hiyo, kwani marehemu alikuwa chini ya gari, huku akiwa hajaumia sehemu yoyote.
Mdogo wa marehemu.
Kwa upande wake mdogo wa marehemu, Stanley Mtikila alisema kuwa, wanaendelea na maandalizi ya mazishi na kubainisha kuwa, marehemu atasafirishwa leo kuelekea Ludewa mkoani Njombe.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana nyumbani kwa marehemu, ilisema mwili wa marehemu utaagwa katika viwanja vya Karemjee jijini Dar es Salaam kwa kuhudhuliwa na viongozi mbalimbali wa chama, Serikali na wadau mbalimbali na kusafirishwa kuelekea nyumbani kwao kwa ajili ya kuzikwa.
Mch.Mtikila alifarika Oktoba 4, mwaka huu kwa ajali ya gari mkoani Pwani.
ciao
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment