MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli,
amesema mabadiliko ya kweli hayawezi kuletwa kwa kuzungusha mikono, bali
yatakuja kwa kufanya kazi.
Kutokana na hali hiyo, amesema yeye ndiye anayeweza kuleta mabadiliko
ya kweli yanayokwenda na vitendo katika kujenga uchumi wa nchi na watu
wake.
Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti, alipokuwa
akizungumza wakati wa mikutano ya kampeni iliyofanyika katika majimbo
ya Buchosa, Geita na Busanda.
Katika mazungumzo yake, Mgufuli aliwataka Watanzania wasidanganywe na baadhi ya wanasiasa wanaowataka wasiipigie kura CCM.
Alisema kwamba, pamoja na baadhi ya wanasiasa kukesha wakihamasisha
mabadiliko kwa kutoichagua CCM, jambo hilo halitawezekana kwa kuwa ni
sawa na ndoto za mchana.
“Ninasema hapa, eti kuna watu wanahangaika kuzungusha mikono na
kusema wanaleta mabadiliko, ni lazima wajue mabadiliko hayawezi kuja kwa
mtindo huo.
“China hivi sasa inatisha kwa kuwa na uchumi wa daraja la kwanza duniani na kuna hatari hata ya kutaka kuizidi Marekani.
“Kwa mfumo wao huo, hawakukiondoa madarakani chama tawala ila walifanya mabadiliko ya ndani ya chama na Serikali.
“Ndiyo maana Magufuli ninakuja na mabadiliko ya kwenda ndani ya
Serikali na ndani ya CCM. Katika hili, sina mchezo ndugu zangu
Watanzania, naomba mniamini,” alisema Dk. Magufuli.
Kwa kuwa Watanzania wameshaamua kumpa urais Oktoba 25, mwaka huu, jambo atakalo anza nalo ni kuunda mahakama ya mafisadi.
Alisema, amezaliwa katika familia maskini na hatakuwa tayari kuona
wajasiriamali wadogo wakinyanyaswa na hata kutozwa ushuru ambao umekuwa
ukiwakandamiza katika biashara zao.
Alisema anajua eneo la Nkome ni maarufu kwa kilimo cha mananasi
daraja la kwanza, lakini bado wakulima wamekuwa wakikosa soko la
uhakika.
Kutokana na hali hiyo, atatimiza mkakati wa Serikali yake kwa kujenga kiwanda cha juisi katika eneo hilo.
“Ni aibu kwa nchi yetu inayozalisha matunda kwa wingi, kukosa kiwanda cha kusindika matunda.
“Napenda kuahidi hapa, nitajenga kiwanda cha juisi kitakachosaidia
wakulima wa mananasi kuwa na soko la uhakika badala ya kwenda Geita
mjini au Mwanza.
“Tukijenga kiwanda hapa, tutatoa ajira kwa vijana na tutatengeneza
juisi yetu badala ya kila siku kuagiza kutoka nje ya nchi, hii ni aibu,”
alisema.
Vita ya Tizeba
Dk. Magufuli aligusia mgogoro wa kifamilia uliopo kati ya mgombea
ubunge wa Jimbo la Buchosa, Dk. Charles Tizeba, anayepigwa vita na
wapinzani wake wakishirikiana na kaka yake wa kuzaliwa.
Alisema anatambua kazi inayofanywa na Dk. Tizeba, hivyo aliwaomba wananchi wa jimbo hilo wamchague kwa kura nyingi.
“Jamani mti wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe maana hapa Buchosa eti
Tizeba anapigwa vita na watu tena hata ndugu yake wa kuzaliwa naye,”
alisema.
Azuru kaburi la babu yake
Akiwa njiani kuelekea katika mkutano wa kampeni katika Jimbo la Geita
Vijijini, Dk. Magufuli alilazimika kwenda katika Kijiji cha Katoma na
kuzuru kaburi la babu yake mzaa baba, Marco Nyahinga, aliyefariki akiwa
na miaka 103.
Katika makaburi hayo, alitembelea pia kaburi la bibi yake mzaa baba, Anastazia Nuhi.
Akizungumza katika makaburi hayo, baba mdogo wa Dk. Magufuli, Simon
Marco, alisema familia imefarijika kwa ujio wa mtoto wao huyo na kwamba
Mungu atamsaidia ili ashinde.
“Tunafurahi sana mtoto wetu amekuwa na kazi kubwa ya kuomba kura kwa
Watanzania, nasi tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu ili ashinde,” alisema.
Kwa upande wake Dk. Magufuli alisema anajua asili yake kwani babu
yake mzee Marco aliwapenda watu wote wakiwemo majirani zake, jambo
ambalo limemsaidia naye kufuata nyayo hizo.
“Hapa Katoma ndipo asili yangu na kitovu changu kilipo, ndipo babu na
baba zangu walipolala, baba yangu maisha yake yote yalikuwa hapa Katoma
kabla hajahamia Chato,” alisema Dk. Magufuli.
Wakati huo huo, Dk. Magufuli alipowasili katika uwanja wa Shule ya
Msingi Ihumilo kwa ajili ya mkutano wa hadhara, alikataa kiti cha
mapambo alichopangiwa na badala yake alikalia kiti cha plastiki.
Kutokana na hali hiyo iliwalazimu wasaidizi wake kupanga viti vya kawaida katika jukwaa na kuvitoa viti maalumu vya mapambo.
0 comments:
Post a Comment