Rais mstaafu wa Nigeria, Gooluck Jonathan, anatarajia kuongoza jopo
la waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuia ya Madola. Huku Rais mstaafu wa
Msumbiji, Armando Guebuza, akiongoza jopo la waangalizi wa Umoja wa
Afrika (AU).
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Balozi Yahya Simba, aliyasema hayo jana wakati akielezea
kuhusu siku ya maadhimisho ya miaka 70 ya kuanzishwa kwa Umoja wa
Mataifa (UN) inayotarajiwa kuadhimishwa Oktoba 13, mwaka huu na kwa
Tanzania yatafanyika jijini Dar es Salaam.
“Rais mstaafu Jonathan ataongoza waangalizi wa Jumuiya hiyo
inayoundwa na nchi wanachama 53 kutoka Afrika, Asia, Amerika, Ulaya na
Pacific,” alisema.
Alifafanua kuwa waangalizi hao wamegawanyika katika makundi mawili moja likiwa la waangalizi na lingine la ukaguzi.
Balozi Simba aliongeza kuwa waangalizi hao wanatarajia kuwasili
nchini siku yoyote kutoka sasa na wataungana na waangalizi wengine
wakiwamo wa Jumuiya ya Ulaya (EU).
Alisema mbali na waangalizi hao, pia kuna waangalizi wengine wengi
wakiwamo wa kutoka nchi za Maziwa Makuu ya Afrika ambao wametuma maombi
kuja kufanya kazi hiyo.
Mratibu Mkaazi wa UN, Alvaro Rodriguez, aliwataka Watanzania
kudumisha amani iliyopo kuelekea uchaguzi mkuu kwa kujifunza kutoka nchi
nyingine ambazo ziko katika machafuko yaliyosababishwa na uchaguzi.
Alisema katika kuelekea maadhimisho ya miaka 70 ya UN yenye kauli
mbiu `Umoja wa Mataifa imara, Dunia bora zaidi, Watanzania wanapaswa
kuendeleza na kuidumisha amani iliyopo.
“Kuna nchi nyingi za Afrika ambazo awali zilikuwa na amani, lakini
kwa sasa ziko katika machafuko na mapigano ya wenyewe, hivyo Watanzania
wasiipeleke nchi yao katika hali hiyo,” alisema Rodriguez.
Alisema UN inasimamia kwa umakini lengo namba 16 linalosema amani kwanza kwa nchi zote duniani.
Alisema pia kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa
kwa UN hapa nchini mbali na ile ya dunia nzima ni `Dunia moja watu
bilioni saba kutunza mazingira ni wajibu wetu.”
Alisema Oktoba 12, mwaka huu kutakuwa na kongamano litakalohusu
vijana wajimbue ili kuchukua uamuzi sahihi kukabiliana na changamoto na
mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.
0 comments:
Post a Comment