BAADA ya kuvunja mwiko wa kutoshinda kwenye Uwanja wa Jamhuri, mkoani
Morogoro kwa misimu mitatu mfululizo, Kocha wa timu ya Yanga, Hans van
Pluijm, amesema kukaa na kuwaelekeza wachezaji wake chakufanya, ndio
sababu kubwa ya kupata matokeo mazuri dhidi ya Mtibwa Sugar.
Yanga tangu msimu wa 2012/ 2013 imekuwa haipati matokeo mazuri zaidi
ya kuambulia pointi moja, iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa
na Malimi Busungu na Donald Ngoma.
Katika msimu wa 2012/2013, Yanga ililala kwa mabao 3-0, msimu uliofuata ikatoka suluhu na msimu uliopita ilifungwa mabao 2-0.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa
juzi, Pluijm alisema alikuwa anaijua historia ya Yanga kwenye uwanja
huo, hivyo aliwaelekeza wachezaji wake nini wanatakiwa kufanya
wanapokuwa uwanjani.
Alisema Mtibwa pia imeponzwa na historia na kusahau kuwa matokeo
hubadilika wakati wowote na kujikuta wakicheza mpira wa nguvu bila
maarifa.
“Nashukuru Mungu vijana wangu walinielewa na wameweza kuvunja uteja
ambao ulikuwa kwa miaka mitatu mfululizo, tumemaliza kazi hapa
tunaangalia mbele tu,” alisema.
Alisema ushindi wa Yanga ulikuwa ni kutoka sare lakini kwa mwaka huu
wameamua kuwaonesha kama wao ndio mabingwa hivyo hakuna siri nyingine ya
ushindi zaidi ya maandalizi mazuri ya kikosi chake.
Pluijm alisema amewapa mapumziko wachezaji wake hadi Jumatatu na
ndipo wataendelea na programu yao ya mazoezi kwa kujifua Uwanja wa Chuo
Cha Polisi Kurasini, Dar es Salaam.
Kutokana na matokeo hayo, Yanga imeendelea kuwa kileleni ikiwa na
pointi 15 sawa na Azam FC iliyo nafasi ya pili ila zinatofautiana kwa
mabao, Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 12 sawa na Mtibwa
wanatofautiana kwa mabao.
0 comments:
Post a Comment