Wanafunzi wamekuwa wakiandamana wiki moja sasa, hasira nyingi zikielekezwa kwa chama tawala African National Congress (ANC).
Mnamo Alhamisi, maelfu ya wanafunzi walikusanyika nje ya makao makuu ya ANC mjini Johannesburg wakitaka elimu itolewe kwa wote bila malipo yoyote.
Vyuo vikuu vimejitetea na kusema vimelazimika kuongeza karo ili kudumisha viwango vinavyohitajika vya ubora wa elimu.
Polisi wamekuwa wakikabiliana na wanafunzi hao katika miji mingi mikuu ya taifa hilo.
Mnamo Alhamisi, watu 29 wamefikishwa mahakamani nchini Afrika Kusini na kushtakiwa kuzua vurugu.
Maandamano hayo ndiyo makubwa zaidi ya wanafunzi tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi 1994.
Polisi kwa mara nyingine walitumia guruneti za kutawanya waandamanaji kuwatawanya wanafunzi mjini Cape Town, siku moja baada yao kuvamia majengo ya bunge.
Maandamano yalianza wiki iliyopita katika chuo kikuu cha kifahari cha Witwatersrand mjini Johannesburg na kuenea katika vyuo vikuu vingine zaidi ya 10.
Vyuo vikuu vingi vilivyokumbwa na machafuko vimefungwa.
Polisi walifanikiwa mara mbili kuzuia wanafunzi hao kufika makao makuu ya chama tawala cha ANC Alhamisi, na kuwalazimisha kurejea vyuoni.
Lakini baadaye waliungana tena na kufika Jumba la Luthuli, ambalo limepewa jina la mshindi wa kwanza wa Tuzo ya Amani ya Nobel Afrika Kusini Albert Luthuli.
Wanafunzi hao walitishia kuandamana tena Ijumaa hadi makao makuu ya serikali mjini Pretoria, ambako Rais Zuma anatarajiwa kukutana na viongozi wa maandamano hayo.
0 comments:
Post a Comment