Imetimia mwezi mmoja kamili tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu
wa Zanzibar, huku viongozi vyama vya CCM na CUF wakiwa na kauli tofauti
kuhusiana na hatma ya uchaguzi huo wakatimazungumzo ya kutafuta muafaka
yakiendelea kugubikwa na siri nzito kutokana na kutotolewa kwa taarifa
yoyote kuhusu mwenendo wa mazungumzo hayo yanayoshirikisha viongozi
wakuu akiwemo Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wake wa
Kwanza Maalim Seif Sharif Hamad.
Jumla ya vikao vinne tayari vimefanyika katika Ikulu ya Zanzibar na
kuwashirikisha viongozi mbalimbali akiwemo Rais Mstaafu wa Tanzania
Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar Dk.Salmin Amour Juma,
Rais mstaafu wa awamu ya sita, Amani Abeid Karume pamoja na Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, lakini hakuna taarifa
yoyote iliyotolewa hadi hivi sasa.
Wakati mazungumzo hayo yakiendelea katika awamu ya nne,Naibu Katibu
Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai amenukuliwa na vyombo vya habari kuwa
suala la kurejewa kwa uchaguzi huo halikwepeki,kutokana na Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar kutangaza rasmi kufuta matokeo hayo katika gazeti
la Serikali.
Vuai amenukuliwa akieleza kuwa shabaha ya mazungumzo hayo ni kuendeleza
amani pamoja na umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Zanzibar, lakini siyo
mbadala wa sheria za uendeshaji nchi na wananchi lazima wapatiwe haki
yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa njia ya
kidemokrasia.
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui ametoa
tahadhari kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kuwa endapo itatangaza
kurejewa kwa uchaguzi mkuu, mazungumzo hayo hayatakuwa na maana tena ya
kuendelea kufanyika, na kusisitiza msimamo wa chama chake kuwa hawako
tayari kurejewa kwa uchaguzi huo.
Zanzibar iliingia katika mgogoro wa kisiasa baada ya Mwenyekiti wa Tume
ya Uchaguzi ya Zanzibar Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi
Mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu, kwa madai ya kugubikwa na kasoro
nyingi ikiwemo udanganyifu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment