WAZIRI MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi maafisa
watano na watumishi watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutokana
na upotevu wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 80/-.
Akizungumza
na viongozi wa Mamlaka ya Bandari pamoja na viongozi wa TRA katika
ziara ya kushtukiza leo mchana (Ijumaa, Novemba 27, 2015), Waziri Mkuu
amewataka Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Rished Bade na Naibu Kamishna Mkuu
wa TRA, Bw. Lusekelo Mwaseba wahahakikishe wanashirikiana na polisi
kufuatilia upotevu huo na kwamba fedha hizo zinapatikana na zinarudi
Serikalini.
Akitangaza uamuzi huo baada ya
kufanya kikao na baadhi ya viongozi wa Serikali bandarini hapo, Waziri
Mkuu aliwataja maafisa waliosimamishwa kazi kuwa ni Kamishna wa Forodha,
Bw. Tiagi Masamaki na Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Bw. Habibu
Mponezya.
“Hawa wanasimamishwa kazi. IGP
ninaagiza hawa watu wakamatwe na kuisaidia polisi. Hati zao za kusafiria
zikamatwe na mali zao zikaguliwe kama zinaendana na utumishi wa umma,”
alisema Waziri Mkuu.
Maafisa wengine
waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa kitengo cha TEHAMA, Bw. Haruni Mpande,
Bw. Hamisi Ali Omari (hakutaja ni wa idara gani), na Mkuu wa Kitengo cha
Bandari Kavu (ICD In-Charge), Bw. Eliachi Mrema. “Hawa wanasimamishwa
kazi hadi uchunguzi utakapokamilika na pia wawe mikononi mwa polisi,”
alisema.
Pia aliagiza watumishi watatu wa
mamlaka hiyo wahamishwe kutoka Dar es Salaam na kupelekwa mikoani.
Watumishi hao ni Bw. Anangisye Mtafya, Bw. Nsajigwa Mwandengele na Bw.
Robert Nyoni.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amemwagiza Katibu Mkuu wa Hazina, Dk. Servacius Likwelile ambaye
alikuwepo kwenye kikao hicho, kuhakikisha kuwa anapeleka wataalamu
kutoka Wakala wa Serikali Mtandao (e-Govt) haraka iwezekanavyo ili
wakakague mifumo ya taarifa na kubaini jinsi ambavyo wizi huo
unafanyika.
“Ninataka uchunguzi uanze
kufanyika mara moja, tafuteni njia ambazo zinatumika kama mianya ya wizi
kutokea hapa bandarini hadi kwenye ICDs. Nataka hayo makontena
yatafutwe hadi yajulikane yako wapi, na fedha hiyo ihakikishwe inarudi
serikalini,” alisema.
Kikao hicho
kilihudhuriwa pia na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Bw. Ernest Mangu,
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Florens Turuka, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Shaaban Mwinjaka, Kamanda wa Polisi Kanda
Maalum ya DSM, Suleiman Kova, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari (TPA),
Bw. Awadh Massawe na viongozi mbalimbali kutoka TRA na TPA.
Mapema
akijibu maswali ya Waziri Mkuu, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Bade alikiri
kwamba kuna upotevu wa makontena ambao huwa unafanyika kati ya bandarini
na ICDs na hasa ICD ya Ubungo. Akitoa ufafanuzi, alisema kwamba
walifanya ukaguzi kwenye ICD moja na kukuta makontena 54 yamepotea kwa
njia za wizi. “Hata hivyo, tulipoendelea na ukaguzi, namba iliongezeka
na kufikia 327. Tunaendelea kufuatilia kwa kushirikiana na TAKUKURU.
Mmiliki wa ICD ametakiwa kulipa faini sh. bilioni 12.6/- na ameshalipa
sh. bilioni 2.4/-,” alifafanua.
Alipoulizwa
na Waziri Mkuu kama ana majina ya watumishi wanaohusika na wizi huo,
Bw. Bade akakiri kwamba anayo lakini siyo kwa wakati huo labda ayapate
kutoka kwa wasaidizi wake. Ndipo Waziri Mkuu akamuonyesha orodha ya
makontena 349 yenye taarifa zote hadi namba za magari yaliyobeba mizigo
hiyo na Bw. Bade akakiri kwamba orodha hiyo ni ya kweli.
“Kwa
utaratibu huo hatuwezi kufika, labda baadhi ya watu waondolewe kazini”.
Ndipo akaanza kutaja majina ya maafisa hao waliosimamishwa kazi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment