JESHI la Polisi nchini limekemea tabia inayoendelea kujengeka
miongoni mwa baadhi ya wananchi ya kutoheshimu sheria na kujichukulia
sheria mikononi kwa kuwapiga, kuwadhalilisha watuhumiwa,kuwachoma na
kuwaua.
Aidha imetangaza zawadi kwa mwananchi yeyote atakayerekodi tukio la
aina hiyo na kulifikisha kwao. Imeelezwa kuwa kuanzia Januari hadi
Oktoba mwaka huu, watuhumiwa 829 wameuawa na wananchi.
Polisi imewaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kukomesha
tabia hiyo na kuahidi kuwa mwananchi yeyote atakayerekodi tukio la watu
wanaojichukulia sheria mkononi na kulifikisha polisi kwa siri atapewa
zawadi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Msemaji wa
jeshi hilo, Advera Bulimba alisema idadi ya watu hao waliokufa
imeongezeka ikilinganishwa na watuhumiwa 785 waliouawa kwa sababu kama
hizo kwa kipindi kama hicho mwaka 2014.
“Katika siku za hivi karibuni, kumeibuka tabia hiyo ya wananchi
kujichukulia sheria mkononi na kuwafanyia vitendo vya kikatili ikiwemo
kuwadhalilisha kwa kuwavua nguo watuhumiwa wanaoshukiwa kujihusisha na
vitendo vya kihalifu bila kuwafikisha kwenye vyombo vya dola jambo
ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi,” alifafanua
msemaji wa Polisi.
Alisema takwimu zinaonesha wazi kwamba tabia hiyo inaendelea
kujengeka na kuonekana kwamba ni jambo la kawaida, lakini ni ukiukwaji
mkubwa wa taratibu na sheria za nchi.
Bulimba alisema makamanda wote wa polisi nchini wameagizwa kufanya
ukamataji wa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu kwa
kisingizio cha hasira kali na kuwafikisha mahakamani kwa sababu watu hao
kwa mujibu wa sheria, tayari wanakuwa wametenda kosa la jinai.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment