Na Lilian Lundo-MAELEZO
Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Mhe. Said Meck Sadiki amesema zoezi la usafi wa mazingira litakalofanyika siku ya Maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, litakuwa ni endelevu kwa mkoa wa Dar es Salaam hata baada ya kumalizika kwa maadhimisho hayo.
Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Tano. Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli aliagiza kuwa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka huu yatumike kwa kufanya usafi wa Mazingira kote nchini badala ya kufanya sherehe za gwaride la askari wa vikosi vya Ulinzi na Usalama.
Akiongea na vyombo vya habari leo Mhe. Sadiki alianza kwa kumpongeza Mhe. Rais
kwa uamuzi aliouchukua wa kubadilisha sherehe za uhuru kuwa ni siku ya kufanya kazi badala ya kwenda uwanjani na kuangalia gwaride na halaiki mbalimbali kama ilivyokuwa ikifanyika miaka iliyopita.
“Mhe.Rais katurejesha kule tulipotoka ambako kauli mbiu ya sherehe za uhuru ilikuwa ni uhuru na kazi au uhuru ni kazi wakati watanzania walikuwa wakiungana na kufanya kazi kwa umoja na kushirikiana,” alisema, Mhe. Sadiki.
Aidha, Mhe Sadiki alisema, zoezi la usafi kwa mkoa wa Dar es Salaam litaanza rasmi tarehe 1 Disemba mwaka huu na kumalizikia 9 Disemba mwaka huu siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya uhuru na kuongeza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu.
Mhe. Sadiki aliongeza kwa kusema kuwa, uongozi wa mkoa umewaomba wadau kujitokeza
kwa kuchangia fedha au vifaa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo na amewataka watendaji kushawishi wananchi wa maeneo yao kutafuta vifaa badala ya kusubiri kuletewa na Halmashauri.
Pia, Mhe Sadiki amewahimiza watendaji wa mitaa na kata kutimiza wajibu wao wa
kuhakikisha maeneo wanayoyasimamia yanakuwa katika hali ya usafi muda wote ili kuepukana na magonjwa ya mlipuko na pale inakapobainika eneo fulani lipo katika mazingira ya uchafu basi mtendaji wa eneo hilo atawajibishwa kwa kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa kosa la
kutotimiza wajibu wake.
Vilevile ametoa wito kwa wananchi kuzingatia usafi kwa kuacha tabia za kutupa taka ovyo hasa wanapokuwa katika vyombo vya usafiri na kutokujisaidia katika mitaro au vichaka ili kuepukana na uchafuzi wa mazingira kunakopelekea kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment