KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ametembelea Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili (MNH) na kuwasilisha maagizo ya Rais John Magufuli
ambayo ni kuwataka madaktari wote nchini, kuhakikisha wanatumia muda wao
kazini na si kufanya mambo yao binafsi.
Pamoja na kuuagiza uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha mashine za
MRI na CT-Scan, zinaanza kufanya kazi mara moja, pia amebainisha kuwa
Serikali ina mpango wa kuongeza mashine mbili za aina hiyo ili kupunguza
mzigo wa wananchi kukosa huduma za vipimo zinazotolewa na mashine hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza ziara yake
hospitalini hapo Dar es Salaam jana, alisema pamoja na madaktari hao,
pia Rais Magufuli, amewataka watumishi wote nchini wa umma, kuwajibika
kwa wananchi ikiwamo kuvaa majina yao ili iwe rahisi kwa wananchi
kuwatambua pindi inapotokea tatizo. “Naomba niwahakikishie na kuwakosoa
wale wote wanaosema kuwa hii ni nguvu ya soda, nawaambie ukweli
tutafuatilia na tumeanza kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari
(Tehama), kudhibiti mapungufu yanayojitokeza katika utoaji wa huduma
kwenye sekta za umma,” alisema Balozi Sefue.
Alisema kwa upande wa madaktari wasiowajibika na kutumia muda wao wa
kazi Serikalini kuhudumia wagonjwa wao binafsi, sasa muda wao umefika na
atakayebainika atachukuliwa hatua za kinidhamu. Aidha, alisema pia Dk
Magufuli amezitaka ofisi zote za umma, kuanzisha madawati ya misaada
yatakayotumiwa na wananchi kwa ajili ya kusaidiwa kupata huduma vizuri
na kuwasilisha malalamiko yao endapo hawatapatiwa huduma kadri
inavyotakiwa.
“Natumia fursa hii kuagiza watumishi wote wa umma, kuvaa majina yao
wakati wanatoa huduma kama ilivyo kwa askari jeshi na polisi, ili
kurejesha imani kwa wananchi, lakini pia kutoa uwazi na fursa kwa
wananchi kuweza kuwatambua wanaowahudumia,” alisisitiza. Balozi Sefue
pia aliitaka Bohari Kuu ya Dawa Tanzania (MSD), kuhakikisha inafungua
maduka ya dawa katika hospitali zote kuu ili kuwasogezea huduma karibu
wananchi, huku akisisitiza kutumika haraka kwa mfumo mpya wa kudhibiti
wizi wa dawa za Serikali. “Rais anataka ule mfumo wa kuweka alama kwenye
dawa za Serikali ufanyike haraka.
Lakini pia natumia fursa hii kuwaonya wenye maduka ya dawa binafsi
watakaothubutu kuuza dawa za Serikali kwani cha moto watakiona,”
alisisitiza. Akizungumzia vitanda vilivyonunuliwa na Bunge kutokana na
agizo la Rais Magufuli la kutumia kiasi cha fedha zilizochangwa kwa
ajili ya hafla ya kuzindua Bunge, Balozi Sefue alisema tayari vitanda
hivyo vimewasili Muhimbili na wagonjwa wote waliokuwa wanalala chini
sasa wamepatiwa vitanda hivyo.
Hata hivyo, alisema amebaini kuwa tatizo hospitalini hapo, halikuwa
ni upungufu wa vitanda pekee, ila kulikuwa hakuna wodi za kutosha kulaza
wagonjwa, ndio maana wagonjwa wengi hasa wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa,
Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI) walikuwa wanalazwa chini
katika wodi nyingine hospitalini hapo. Alisema tayari taasisi hiyo
inatarajia kukamilisha jengo lake jipya na la kisasa ambalo pamoja na
kuwa na wodi, pia litakuwa na huduma za vipimo vya MRI na CT-Scan, hali
itakayosaidia pia kupunguza matatizo ya vipimo hivyo hospitalini hapo.
Aidha, Sefue alitumia fursa hiyo kuzitaka hospitali zote nchini,
kuhakikisha kuwa zinatengeneza mfumo bora wa kufanyia marekebisho
mashine zote zinazotumika katika huduma za afya na kuepuka kutupia mzigo
wa gharama za matengenezo hayo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
“Kuanzia sasa mikataba yote ambayo taasisi za umma zitaingia kwa
ajili ya ununuzi wa vifaa au mashine zinazotoa huduma, lazima iwe na
kipengele cha kampuni zinazouza vifaa hivyo, kuhakikisha wanatoa elimu
kwa wataalamu Watanzania ili kuepuka gharama kubwa za matengenezo,”
alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk
Donan Mmbando, alisema tayari Serikali imeingia mkataba na nchi ya
Uholanzi kupitia Kampuni ya Philips kwa ajili ya kuagiza mashine zaidi
ya MRI na CT-Scan ambazo zitatumika katika jengo jipya la MOI. “Pia
kupitia mapendekezo yetu ya bajeti inayokuja tumeomba tupatiwe kiasi cha
Sh bilioni 12, kwa ajili ya kufanyia ukarabati wa maeneo mbalimbali ya
kutolea huduma za afya katika hospitali zetu kuu, lengo likiwa ni
kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za afya,” alisisitiza.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema tayari
wamewasilisha vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 251 kwa MNH kupitia MOI
ambavyo ni vitanda na magodoro 300, viti maalumu vya wagonjwa 30,
vitanda maalumu vya kubebea wagonjwa 30, shuka 1,695 na mablanketi 400.
Home
News
Serikali ya Magufuli yawaonya Madaktari nchini kufanya kazi na kuacha kufanya mambo yao binafsi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment