Image
Image

Mshambuliaji Amis Tambwe ameshindwa kuanza mazoezi kutokana na maumivu ya shingo.

WAKATI kikosi cha Yanga kinatarajia kuingia kambini Jumatatu ijayo kujiandaa na michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayofanyika mkoani Tanga, mshambuliaji Amis Tambwe ameshindwa kuanza mazoezi kutokana na maumivu ya shingo.
Yanga itacheza mchezo wa raundi ya 10 dhidi ya Mgambo Shooting Desemba 12 mwaka huu Uwanja wa Mkwakwani Tanga, kisha siku chache baadaye itacheza na African Sports kwenye uwanja huohuo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Yanga Hans Pluijm alisema hadi kufika Jumatatu wachezaji wake wengi watakuwa wameunganika tayari kwa maandalizi kuelekea mchezo wao ujao.
Jana wachezaji wa Yanga waliendelea na mazoezi katika uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam, lakini Tambwe aliyekuwepo mazoezini hapo alikuwa mtazamaji huku akiwa amefungwa kifaa tiba maalumu shingoni kutokana na matatizo ya shingo yanayomkabili.
Akizungumza na gazeti hili, Tambwe alisema huwa shingo wakati mwingine inamsumbua, ingawa si kwa kiwango cha kuogopa. “Lakini naamini nitakaa vizuri tu baada ya kupata matibabu,” alisema Tambwe.
Licha ya Tambwe, wachezaji Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Haji Mwinyi na Oscar Joshua nao jana walishindwa kufanya mazoezi kutokana na majeraha yanayowakabili. Walifanya mazoezi mepesi kutokana na kuwa majeraha waliyopata wakiwa na timu ya Zanzibar katika mashindano ya Chalenji yanayoendelea nchini Ethiopia.
Joshua ameumia kifundo cha mguu. Akizungumzia hali zao daktari wa timu hiyo, Haruni Ally alisema zinaendelea vizuri na anatarajia pengine Jumatatu watakuwa wamepona na kujumuika kufanya mazoezi na wenzao isipokuwa Joshua.
“Wanaendelea vizuri, Cannavaro na Mwinyi wapo kwenye tiba na hali zao zinaendelea kuimarika na Tambwe shingo yake ina matatizo kidogo, lakini mpaka Jumatatu atakuwa kwenye mazoezi pamoja na wenzake isipokuwa Joshua yeye anaweza kuuguza kifundo kwa wiki mbili”, alisema Ally.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment