Image
Image

Nivema Serikali iboreshe shule zake badala ya kuzibana za binafsi.

Serikali imepiga marufuku ongezeko la ada kwa shule binafsi kuanzia Januari, mwakani na kuwataka wamiliki na wakuu wa shule hizo kuzingatia Waraka wa Elimu namba 4 wa mwaka 2008.

Waraka huo uliweka viwango vya ada zinazotozwa katika shule za msingi na sekondari kwa zile za serikali na binafsi.

Serikali imeeleza kuwa iko katika hatua za mwisho za utafiti na kuandaa mfumo wa kielektroniki wa kutambua gharama za elimu ya msingi hadi kidato cha nne ili kuwa na ada elekezi kwa shule zote.

Viwango vinavyotakiwa na serikali ni Sh. 150,000 kwa shule za kutwa wakati Sh. 380,000 kwa shule za bweni.

Waraka wa serikali unaelekeza kuwa shule zinatakiwa kupata kibali cha serikali pale zinapotaka kuongeza ada.

Hata hivyo, jambo hilo limezua balaa kwani wamiliki wa shule binafsi wametishia kutofungua shule zao kutokana na azma hiyo ya serikali.

Serikali inaeleza kuwa imefikia uamuzi huo baada kugundua kuwa shule nyingi za binafsi zimekuwa na utaratibu wa kupandisha ada zake kila mwaka.

Kitendo cha kupandishwa kwa ada mara kwa mara kwa baadhi ya shule kimesababisha baadhi ya wazazi kushindwa kusomesha watoto wao.

Hata hivyo, kimsingi tunaelewa dhamira njema ya serikali katika kudhibiti ada za kiwango cha juu kwa shule binafsi, lakini jambo hili linatakiwa kuangalia kwa mapana yake.

Serikali inapaswa kujua chanzo cha shule za binafsi kuwa kiwango cha juu cha ada.

Suala la shule za binafsi kupanda ada, limechangiwa kwa kiasi kikubwa na serikali kushindwa kuendesha shule zake ipasavyo.

Katika miaka ya nyuma, lilikuwa jambo la fahari kwa mzazi kumsomesha mtoto wake katika shule ya serikali.

Katika miaka hiyo, kila mzazi alipenda mtoto wake asome shule za sekondari, mathalani Ilboru, Umbwe, Milambo, Tabora, Weruweru, Rugambwa, Malangali, Bwiru na nyinginezo.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, hali iko tofauti kutokana na ukweli kuwa siyo shule za serikali ziko katika hali mbaya.

Kwa sasa wazazi wengi wameelekeza nguvu zao kusomesha watoto wao kwenye shule za binafsi.

Na ushahidi ulio wazi ni jinsi wanafunzi wa shule binafsi wanavyofanya vizuri katika mitihani mbalimbali ya kitaifa.

Sasa ni jambo la kusikitisha kuona kuwa serikali inaingilia uendeshaji wa shule binafsi wakati imeshindwa kusimamia shule zake.

Dawa ya kudhibiti tatizo la kupanda kwa ada za shule za binafsi ni kwa serikali kuboresha shule zake ili zitoe kiwango bora cha elimu.

Watendaji wenye dhamana ya kusimamia sekta ya elimu nchini wanapaswa kukumbuka ule msemo wa Kiswahili unaosema `kizuri chajiuza na kibaya chajitembeza.'

Ukweli upo kuwa kuna shule zinatoza ada ya juu sana, lakini hili limechangiwa zaidi na serikali kushindwa kutoa elimu ya kiwango bora.

Mathalani serikali ya awamu ya nne ilikuja na mpango kamambe wa kujenga shule katika kila kata.

Ni kweli shule zilijengwa kwa kasi, lakini jambo la kusikitisha ni kuwa shule zenyewe zina matatizo makubwa ikiwamo uhaba wa walimu na vifaa vya kufundishia.

Tunashauri serikali ikae na wamiliki wa shule ili kupata ufumbuzi ambao utakuwa wa manufaa kwa pande zote mbili.

Tukumbuke uendeshaji wa shule una gharama zake na pia serikali inapaswa kujua kuna suala la soko huria kwenye sekta binafsi, sasa badala ya kuzibana shule binafsi iboreshe shule zake.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment