MAWAZIRI wawili wametumbuliwa majipu’ baada ya
kutangaza kusimamishwa kazi kwa Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Mabasi yaendayo
Haraka (DART), Asteria Mlambo na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya
Ocean Road, Dk Diwani Msemo, wote wakipisha uchunguzi dhidi yao.
Mlambo amesimamishwa kazi kuanzia jana ili kupisha
uchunguzi baada ya serikali kubaini ukiukwaji wa wazi wa Sheria ya Manunuzi ya
Umma katika kumpata mtoa huduma ya mpito wa mradi huo wenye nia ya kupunguza
msongamano wa magari barabarani kwa madhumuni ya kurahisisha usafiri na
usafirishaji jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George
Simbachawene alisema kutokana na kukamilika kwa sehemu ya ujenzi wa miundombinu
ya Awamu ya Kwanza ya mradi, Serikali iliamua kuwa na mtoa huduma wa mpito
kabla ya kumpata wa kudumu.
“Mtoa huduma wa mpito alipaswa kupatikana kwa mujibu wa
Sheria ya Manunuzi ya Umma. Hata hivyo, Serikali imebaini ukiukwaji wa wazi wa
sheria hiyo wakati wa kumpata mtoa huduma wa kipindi cha mpito.
“Kufuatia hali hiyo nimeamua kumsimamisha kazi kuanzia
leo tarehe 23 Desemba, 2015, Mtendaji Mkuu wa DART, Bi. Asteria Mlambo ili
kupisha uchunguzi,” alieleza Simbachawene.
Simbachawene alizitaja sababu za kumsimamisha kazi
Mtendaji Mkuu huyo wa DART kuwa ni kushindwa kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya
Umma wakati wa kumpata mtoa huduma katika kipindi cha mpito; kushindwa kuchukua
hatua hata pale alipobaini kuwa mtoa huduma wa mpito amekiuka masharti ya
mkataba wa kutoa huduma ya mpito; na kufanya maamuzi makubwa pasipo
kuishirikisha Bodi ya Ushauri ya DART.
Aidha, alisema Serikali inatambua kuwa wapo watumishi wa
DART ambao hawakumshauri vizuri Mtendaji Mkuu, hivyo watumishi hao
watachunguzwa na kuchukuliwa hatua na Kaimu Mtendaji Mkuu atakayeteuliwa.
“Nimemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi kuendelea
na taratibu za kinidhamu dhidi ya Mtendaji Mkuu aliyesimamishwa kazi,” alisema
Simbachawene. Aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua
kwa haraka na uangalifu ili mradi huu uanze kutoa huduma bora ya usafiri kwa
wakazi wa Dar es Salaam bila kuchelewa zaidi, huku akiwaomba kuitunza na
kuithamini miundombinu ya DART kwa kuwa imegharimu fedha nyingi kwa manufaa
yao.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea
maeneo ya mradi huo wa DART na kuagiza kuwa uanze kazi Januari 10, mwakani
baada ya kupigwa kalenda kwa muda sasa tangu mwaka jana.
Wakati Simbachawene akichukua hatua hiyo, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amemsimamisha Dk
Msemo kwa kile kilichoelezwa ni kupisha uchunguzi unaolenga kubaini iwapo
mgongano wa kimaslahi umeathiri utendaji wa taasisi hiyo.
Aidha, watendaji wote wa serikali katika sekta ya afya
hususan wakuu wa vituo vya kutolea huduma za afya, wafamasia, wauguzi na
waganga wafawidhi, wameagizwa kukiri kwa maandishi ndani ya siku 21 kuanzia
sasa endapo wanamiliki hospitali, zahanati, kliniki na maduka ya dawa.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Waziri
Mwalimu, imefafanua uamuzi wa kumsimamisha Kaimu Mkurugenzi huyo wa Ocean Road,
unatokana na ziara walizofanya kukagua utoaji wa huduma za afya katika maeneo mbalimbali
ambako walibaini upungufu wa dawa umeendelea kujitokeza kwa wingi.
“Baadhi ya wagonjwa walieleza kwa uchungu jinsi
wanavyopata tabu ya kupata dawa hata zile ambazo wanatakiwa wazipate kwa bei ya
ruzuku au zinazotakiwa kutolewa bure na serikali,” ilisema taarifa hiyo.
“Kwa kuzingatia suala hili la mgongano wa kimaslahi,
manung’uniko mengi kutoka kwa wapokea huduma, hususan katika Taasisi yetu ya
Saratani ya Ocean Road, nimechukua hatua ya kumsimamisha kazi Kaimu
Mkurugenzi,” iliongeza taarifa ya waziri huyo.
Waziri alisema lengo ni kupisha uchunguzi pamoja na mambo
mengine kubaini iwapo mgongano wa kimaslahi umeathiri utendaji wa taasisi chini
ya kaimu mkurugenzi huyo.
Ingawa haikufafanuliwa mgongano wa maslahi na uhusiano wa
utendaji wa Dk Msemo, Waziri alisema anatambua kuwa Serikali iliridhia
watumishi wa sekta ya afya kumiliki vituo vya kutolea huduma za afya na maduka
ya dawa.
Hata hivyo, alisema umiliki huo unaleta hisia kwa
wananchi kwa misingi ya mgongano wa kimaslahi. Kuhusu watendaji wa sekta ya
afya kutakiwa kukiri kwa maandishi kuhusu umiliki wao wa hospitali, zahanati,
kliniki na maduka ya dawa, Waziri Mwalimu alisema hatua hiyo inalenga kusaidia
kuziba mianya ya upotevu wa dawa, vifaa na vifaa tiba katika vituo vya umma.
Alisema hatua hiyo pia itarejesha imani ya wananchi kwa
watumishi wa umma wanaohusika moja kwa moja na utoaji wa huduma za afya nchini.
Alisema agizo hilo la jana, halimwondolei wajibu kiongozi yeyote wa Serikali
ambaye anapaswa kujaza tamko la viongozi wa umma kuhusu rasilimali na madeni
kwa mujibu wa Kifungu cha 9 na 11 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma
Namba 13 ya mwaka 1995 na Namba 5 ya mwaka 2001.
0 comments:
Post a Comment