WATU wawili wakiwemo Mwanasheria na Mwalimu, wamepandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na
mashitaka ya kula njama za kumuua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva na familia yake.
Washitakiwa hao, Mwalimu Samwel Gikaro (30) na Mwanasheria Angela
Mbonde (32) walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka
mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba.
Wakili wa Serikali, Hellen Moshi alidai kati ya Oktoba 23 na Novemba
16, mwaka huu katika maeneo tofauti Dar es Salaam na maeneo mengine
nchini, washitakiwa na wengine ambao hawajafika mahakamani, walikula
njama za kumuua Jaji Lubuva na familia yake.
Washitakiwa walikana mashitaka na upande wa Jamhuri ulidai kuwa
upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Wakili wa upande wa utetezi, Moses Kaluwa ambaye alifika mahakamani hapo
kwa niaba ya Wakili Peter Kibatala, aliiomba mahakama itoe dhamana kwa
washitakiwa kwa kuwa mashitaka yanayowakabili yana dhamana.
Wakili Moshi alidai Jamhuri inatambua mashitaka hayo yana dhamana
kisheria, lakini inaomba dhamana izuiliwe kwa muda hadi watakapoona
inafaa kwa sababu ya asili ya kosa, washitakiwa hawawezi kuwa nje wakati
upelelezi unaendelea.
Hata hivyo, Wakili Kaluwa alidai sababu zilizotolewa na upande wa
jamhuri hazina msingi kisheria, suala la msingi ni mashitaka
yanayowakabili kuwa na dhamana na washitakiwa wapo tayari kutimiza
masharti yatakayotolewa na mahakama.
Hakimu Simba alisema pamoja na mashitaka hayo kuwa na dhamana
kisheria, kutokana na kosa pamoja na hatua ya upelelezi, mahakama
imekubali hoja za upande wa jamhuri hivyo washitakiwa watakuwa rumande.
Kesi itatajwa tena Desemba 15, mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment