KOCHA wa muda wa Simba, Jackson Mayanja amesema bado
ana kazi kubwa ya kufanya kubadili mfumo wa uchezaji wa timu hiyo ili kuleta
burudani kwa mashabiki na wanachama wa timu hiyo.
Mayanja aliyechukua mikoba ya Dylan Kerr aliyefutwa
kazi wiki iliyopita, ameanza vyema kibarua chake kwa kuiongoza Simba kushinda
bao 1-0, dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu mzunguko wa 14,
uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam juzi.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa pambano hilo
Mayanja, alisema amefurahi kuanza vizuri kibarua chake lakini bado ana kazi ya
kufanya kuhakikisha timu hiyo inaonesha kiwango cha kuvutia na ushindi kwa
sababu ni timu kubwa Tanzania.
“Tumefanya mazoezi kwa siku tatu kabla ya mchezo wa
leo (juzi), lakini nimefurahi kuona mabadiliko kidogo tofauti na ilivyokuwa
mwanzo, lakini bado sijaridhika nataka kuongeza wingi wa mazoezi ili kuwaweka
fiti wachezaji wangu ili siyo tu tupate ushindi, lakini pia tuoneshe kiwango
cha kuvutia kwa sababu Simba ni timu kubwa Tanzania,” alisema Mayanja.
Kocha huyo raia wa Uganda alisema kazi ya kuwaweka
fiti wachezaji wake amepanga kuifanya taratibu ili asiwachanganye na kofia
kuwachosha wakashindwa kutimiza majukumu yao katika mechi za Ligi Kuu.
Kwa upande wake kocha wa Mtibwa Sugar Mecky Maxime,
aliwapongeza wachezaji wake kwa kuonesha kiwango kizuri ingawa hawakuweza
kusawazisha bao hilo la mapema lililofungwa dakika ya sita na Hamisi Kiiza.
Maxime, alisema uchovu ndiyo kitu kikubwa
kilichosababisha kupoteza mchezo huo lakini kitu pekee anachojivunia ni kwamba
timu yake haikupoteza shepu ya uchezaji, licha ya uchovu waliokuwa nao
uliotokana na fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya URA ya Uganda
wiki iliyopita.
Maxime alisema licha ya kupoteza mchezo huo, bado
lengo lao lipo palepale kuhakikisha msimu huu wanapambana kupigania ubingwa wa
Ligi Kuu Tanzania Bara, kama ilivyokuwa msimu wa mwaka 1999 na 2000.
0 comments:
Post a Comment