Wanajeshi wa Kenya waliojeruhiwa kwenye shambulio
lililofanywa na wapiganaji wa al shabaab katika eneo la el adde wamesafirishwa
hadi Nairobi.
Wapiganaji hao wa Al shabaab walishambulia kambi ya
jeshi la umoja wa mataifa nchini Somalia na kuna ripoti kuwa wanajeshi kadhaa
wa Kenya waliuawa huku wengine wakijeruhiwa.
Idadi ya wanajeshi waliouawa haijabainika wazi
lakini kundi hilo la Al shabaab linadai kuwa liliwauwa zaidi ya wanajeshi
sitini madai ambayo serikali ya Kenya imekanusha.
Miongoni mwa waliokuwa kwenye uwanja wa ndege wa
Wilson kuwalaki wanajeshi hao waliojeruhiwa ni pamoja na waziri wa ulinzi Bi
Rachael Omamo na maafisa wengine wa ngazi ya juu jeshini na serikalini.
Omamo amesema habari kuhusu wanajeshi walioangamia
zitawasilishwa kwa familia zao moja kwa moja.
Aidha amesema wanajeshi wa Kenya bado wangali
wanapambana na wapiganaji hao wa Al shabaab ili kujaribu kuwakomboa wanajeshi
waliokwama ikiwa wapo.
Kenya imekariri kuwa haitaondoa wanajeshi wake
Somalia hadi pale kundi hilo la al shabaab litakaposambaratishwa kabisa na
amani kurejea nchini humo.
Wakati huo huo kundi hilo limedai kuwa
linawashikilia wanajeshi kadhaa wa Kenya mateka.
Al Shabaab limesema ni mara ya kwanza kikosi chake
maalum cha Saleh ali saleh Nabhan kilifanya shambulio ndani ya somalia.
Saleh ali Saleh Nabhan alikuwa kiongozia wa Al qaeda
katika kanda ya Afrika mashariki na aliuawa kwenye shambulio lililofanywa na
Marekani mwaka wa 2008
Tangu mwaka wa 2011 wakati Kenya ilituma wanajeshi
wake nchini Somalia, kundi hilo limefanya mashambulio kadhaa ya kigaidi nchini
Kenya na kusababisha maafa makubwa.
0 comments:
Post a Comment