GAZETI hili jana lilichapisha habari iliyokuwa na
kichwa cha habari “TRA yakusanya Shilingi trilioni 1.7 kwa mwezi.”
Hii ni kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) na kuonesha kwa uwazi uhalisia wa makusanyo hayo kutoka kwa
walipa kodi.
Tulizoea kusikia hesabu ya mamilioni na bilioni,
lakini kwa kasi na juhudi mpya tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu
ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, kuna kila dalili ya kusahau
makusanyo ya mamilioni na bilioni na kwenda katika hatua nyingine ya trilioni,
lugha ambayo imeanza kuzoeleka na kusikika kwenye masikio ya watanzania wengi,
tofauti na hapo awali.
Hakuna ubishi kwamba matunda hayo ya trilioni, tunazosikia
zinatokana na juhudi za wazi na za makusudi ya dhamira ya serikali ya
kuhakikisha mapato, yanakusanywa kwa umakini mkubwa kwa kumhusisha kila
anayestahiki kulipa kodi anafanya hivyo, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi ambao
mara nyingi uwezekano wa kukwepa kulipa kodi huwa ni mdogo.
Wote ni mashahidi kwamba kasi mpya ya kuziba mianya
ya wakwepa kulipa kodi kutoka bandarini, TRA na wafanyabiashara wasio waaminifu
ndiko kunakotufikisha katika hatua hii ya mafanikio ya kufikia makusanyo ya
trilioni.
Tunapenda kuchukua fursa hii, kuwapongeza wenzetu wa
TRA na serikali kwa ujumla wake, kwa kulivalia njuga suala hili nyeti kwa uhai
na ustawi wa watanzania wote kwa kukusanya kodi kwa mujibu wa sheria na
taratibu.
Tuna imani kwamba hali ya makusanyo, itaendelea
kung’ara kwa miezi ijayo, ukizingatia kwamba Jeshi letu la Polisi limerejeshwa
tena katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kuhakikisha kwamba mianya
iliyotumika na wajanja wachache kuhujumu makusanyo, ikiwa ni pamoja na
makontena kwa maelfu kuondolewa bandarini bila kulipia kodi, sasa itadhibitiwa
ipasavyo.
Sote ni mashuhuda kwa habari tuliyochapisha jana,
iliyomkariri Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Silvarius Likwelile
akieleza kuwa fedha zilizokusanya, zimekwishasambazwa kulipia huduma mbalimbali
za jamii kwa mabilioni.
Miongoni mwa maeneo ambako mabilioni hayo
yamepelekwa ni Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), utoaji wa elimu bure, mikopo
kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kuwajengea uwezo walimu, mipango ya maji
vijijini, ujenzi wa barabara, miradi ya umeme vijijini, maendeleo ya mahakama
na upanuzi wa udahili wa wanafunzi kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Tunadiriki kusema kwamba haijawahi kutokea serikali
ikatoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kiwango cha
mabilioni na kwa uwazi kiasi hiki. Tumefikia hatua hiyo kubwa kutokana na
makusanyo ya uhakika ya kodi. Kinyume chake, tungekuwa tunaendelea kusubiri
wahisani wa kutupatia misaada.
Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli
imeshatamka wazi kwamba haitaki kuwa ombaomba kutokana na ukweli kwamba nchi
imejaliwa rasilimali za kutosha.
Iwapo tutatumia rasilimali hizo kwa umakini na kwa
uadilifu na kuchapa kazi bila kufanya ajizi, ikiwemo kujenga viwanda na kutumia
vizuri rasilimali za gesi na mafuta, Tanzania itaweza kuingia katika uchumi wa
kati hivi karibuni. Tusikubali kurudi nyuma. Tuendelee kupambana. Mungu Ibariki
Tanzania.
0 comments:
Post a Comment