NAIBU WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
anayeshughulikia Mazingira, Bw.Luhaga Mpina amesema mkoa wa Simiyu ni miongoni
mwa mikoa nane hapa nchini ambayo inakabiliwa na tishio la kugeuka jangwa
kutokana na tatizo la ukataji miti hovyo.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Simiyu, Mwanza, Mara,
Singida na Arusha. Mingine ni Kilimanjaro, Dodoma na Manyara.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Machi 2,
2016) alipopewa nafasi na waziri Mkuu Kassim Majaliwa awasalimie wananchi
waliofika kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi kwenye jengo la utawala la
Halmashauri ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu.
Alisema kila wilaya imepewa agizo la kupanda miche
milioni 1.5 kwa mwaka na kwa sababu hiyo watawapima wakuu wa mikoa, wakuu wa
wilaya na wakurudenzi wa halmashauri na Manispaa ambao hawatafikisha idadi hiyo
ya miche na kuwasilisha majina yao kwa Waziri Mkuu.
"Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeagiza kila
wilaya ipade miche milioni 1.5 kwa mwaka. Kwa hiyo kuanzia Machi 3, mwaka
ambayo ni siku ya upandaji miti, tutawamoniter Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa
Wilaya wote ili kubaini ni nani hajatekeleza agizo hili. Tutakuletea mezani
kwako majina ya wale ambao watashindwa kutekeleza agizo hili ambalo liko kwenye
Ilana ya CCM," alisema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri huyo alisema amekuja
na miche 7,000 ya matunda aina ya miembe, michungwa na mifenesi ambayo ameahidi
kuigawa kwa kila wilaya. "Tunataka katika ziara yako hii tusambaze miche
5,000 kwa kila jimbo la mkoa huu na wakati unamaliza ziara yako tutakuwa
tumesambaza miche 35,000," alisema.
Naibu waziri Mpina alisema kupandwa kwa miti
mbalimbali ya matunda, kutawasaidia wananchi kupata matunda ya kula, ya kuuza
na kupata fedha lakini pia itawasaidia kuwa chanzo cha mali ghafi kwenye
viwanda vya kusindika matunda.

0 comments:
Post a Comment