Wanaharakati wa haki za binaadamu na jumuiya za waandishi wa
habari nchini Tanzania wametoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa mwandishi wa
habari wa magazeti ya Mwananchi Communications na mwakilishi wa Deutsche Welle
visiwani Zanzibar, Salma Said, ambaye ametoweka tangu jana katika mazingira ya
kutatanisha.
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari (UTPC) umesema
unapingana na kitendo hicho ambacho umesema kinarejesha nyuma jitihada za
waandishi kufanya kazi zao.
Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Abubakar Karsan, ameiambia DW
kwa njia ya simu kwamba kukamatwa kwa Salma katika mazingira yasiyoeleweka ni
hatari kwa uhuru wa habari. "Huku ni kumtisha ili asifanye kazi yake ya
uandishi kwa haki na uadilifu na haikubaliki. Serikali inaonekana kutumia nguvu
sana dhidi ya waandishi kama yeye na hivyo si sawa. Tutasimama pamoja naye na
tunataka aachiliwe mara moja."
Katika ujumbe wake, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu
nchini humo (THRD) umesema kupitia ukurasa wake wa Facebook kuwa unalaani
vikali kutekwa kwa mwandishi huyo wa kike na kuvitolea wito vyombo vya usalama
"kutoa ushirikiano katika kipindi hiki" na pia kuwataka waandishi wa
habari "kuungana ili kushinikiza" apatikane haraka.
Salma Said mwenye umri wa miaka 45 alitoweka jana visiwani
Zanzibar katika mazingira ya kutatanisha na hadi sasa bado familia yake haijui
alipo.
0 comments:
Post a Comment