Image
Image

Mauaji ya Imamu na waumini msikitini Mwanza sikitendo cha kiungwana ni unyama.

JUZI usiku watu wasiojulikana waliwaua watu watatu akiwamo imamu msaidizi wakati walipokuwa wakiswali katika msikiti uliopo Ibanda Relini, Mtaa wa Utemini katika Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana, jijini Mwanza.

Imeelezwa kuwa watu hao waliuawa kwa kukatwa katwa mapanga na kundi la watu zaidi ya 15. 
Waliouawa katika tukio hilo ni Ferouz Elias, Imamu wa msikiti huo, Mbwana Rajab na Khamis Mponda ambaye ni dereva bodaboda huku Ismail Abeid, mwanafunzi wa Shule ya Kiislam ya Jabar iliopo Nyasaka jijini humo akijeruhiwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema watu wasiojulikana waliuvamia msikiti huo majira ya saa 2:00 usiku na kuwachinja watu watatu waliokuwa wakiswali swala ya saa mbili na kwamba wahalifu hao waliwaamuru watoto waliokuwapo ndani ya msikiti wakimbie ili watimize matakwa yao.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wanasema kuwa watu hao walipouvamia msikiti huo wakiwa wamefunika sura zao huku wakiwa na bendera ya kundi la kigaidi la Dola ya Kiislamu (IS), waliwaamuru watu wote waliokuwa msikitini kulala chini na baada ya hapo walimuita Imamu wakimuita msaliti kutokana na kitendo cha kuswalisha wakati Waislamu wengine wanasaidiana na IS kupigana vita katika nchi mbalimbali na baada ya hapo walianza kutekeleza unyama huo.
Habari zaidi kutoka kwa mashuhuda zinaeleza kuwa wauaji hao walikuwa na bunduki pamoja na mabomu ya moto ya kutengeneza na kwamba, walirusha mabomu hayo, lakini hayakuleta madhara yoyote.
Tunakilaani kitendo hicho cha mauaji ya kinyama dhidi ya watu waliokuwa katika nyumba ya ibada wakimwabudu mwenyezi Mungu na kimsingi hakipaswi kupewa nafasi nchini. Tukio hilo ni mwendelezo wa vitendo vyenye sura ya ugaidi katika miaka ya karibuni na kutokea katika nyumba za ibada au kuwalenga viongozi wa dini.
Oktoba 2012, makanisa sita yalichomwa moto jijini Dar es Salaam kwa siku moja eneo la Mbagala wilayani Temeke; Novemba 2012 lilifanyika shambulio dhidi ya imam mmoja mwenye msimamo wa wastani visiwani Zanzibar; Desemba 2012 Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mpendae Zanzibar alipigwa risasi wakati anafungua geti ili aweze kuingia nyumbani kwake eneo la Kitomondo na Februari 2013 Padri wa Kanisa Katoliki Minara Miwili Zanzibar, Evarist Mushi aliuawa kwa kupigwa risasi.
Mei 2013 Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti lilishambuliwa kwa bomu jijini Arusha na watu watatu walifariki dunia na wengine 63 kujeruhiwa.
Kauli wanayodaiwa kuitoa waliofanya unyama wa Mwanza juzi na kubeba bendera ya IS ni jambo linaloacha shaka na kuhitaji kufuatiliwa.
Pamoja na Kamanda Msangi kusema kuwa watu watatu wametiwa mbaroni kuhusiana na tukio la Tanga, tunawakumbusha Watanzani kuwa kila mmoja ana wajibu wa kuwa mlinzi wa usalama na jambo la msingi ni kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pale wanapoona kuna watu wasiowafahamu katika mazingira ya kutia shaka.
Suala la kuabudu ni haki ya kila raia na nchi yetu na haki ya kila Mtanzania kuabudu dini anayoitaka bila kuzuiwa na mtu au kikundi chochote inalindwa na Katiba ya nchi.
Kutokana na taarifa za tahadhari za uwezekano wa kujipenyeza makundi ya kigaidi katika eneo la Ukanda wa Afrika Mashariki, tunavikumbusha vyombo vyetu vya dola kuhakikisha vinachukua tahadhari wakati wote kudhibiti vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment