SERIKALI
imetangaza kuboresha hospitali za rufaa, maalumu, za kanda na Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambayo sasa itaanza kutoa huduma ya
kupandikiza figo. Aidha, itajenga jengo maalumu la kulaza viongozi wa
kitaifa na watu mashuhuri.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hayo bungeni mjini hapa
jana alipokuwa akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa
fedha 2016/2017.
Alibainisha kuwa maboresho hayo kwa upande wa MNH
ni pamoja na kuongeza idadi ya vitanda vya wagonjwa wenye kuhitaji
uangalizi maalumu (ICU) kutoka 21 hadi vitanda 75.
Pia itanunua vifaa
tiba vya upasuaji na kuongeza vyumba vya upasuaji kutoka 13 vya sasa
hadi 18, itapanua huduma za kusafisha figo kwa kuongeza vitanda kutoka
15 hadi vitanda 50 na kuanza kusafisha figo kwa wagonjwa wenye Virusi
Vya Ukimwi na virusi vya ini.
“Muhimbili itaanzisha huduma mpya ya
upandikizaji figo na upandikizaji wa ‘cochlea’ kwa wagonjwa ambao ni
viziwi…itajenga jengo la kisasa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa
binafsi na viongozi wa kitaifa na watu mashuhuri litakalokuwa na vitanda
170 na kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 2.6 za sasa hadi
shilingi bilioni tano kwa mwezi,” alisema Ummy.
Alisema Taasisi ya
Mifupa Muhimbili (MOI) katika mwaka wa fedha 2016/2017, itaongeza nafasi
ya wagonjwa wanaolazwa kutoka vitanda 150 hadi 340 ambapo katika chumba
cha wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU) vitaongezeka kutoka
vinane hadi 32.
“Serikali itanunua mashine mpya za uchunguzi ikiwa
ni pamoja na MRI, CT scan na Xray za dijitali. MOI itatoa mafunzo na
upasuaji wa marejeo kwa nyonga na goti,” alifafanua.
Kwa upande wa
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambayo mwaka wa fedha 2015/2016
ilihudumia wagonjwa 24,570 wa nje na waliolazwa 2,134, alisema katika
mwaka ujao wa fedha wizara itaijengea uwezo taasisi hiyo kwa kuweka
vifaa ili chumba cha upasuaji cha tatu kianze kufanya kazi.
Waziri
huyo alisema huduma za kibingwa za mkoba (outreach services) zitatolewa
katika hospitali za Temeke, Amana, Mwananyamala (zote za Dar es Salaam),
Tumbi mkoani Pwani na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Kwa
upande wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, alisema katika mwaka wa
fedha 2016/2017 itapatiwa vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu
ikiwa ni pamoja na PET/CT scan, Linac na MRI.
Pia itatoa huduma za
mkoba hasa katika maeneo yatakayoonekana kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa
wenye saratani. “Wizara itaimarisha upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa wa
saratani ambapo asilimia 13 ya fedha za dawa zitatumika kununua dawa za
saratani ili kupunguza mzigo kwa wagonjwa hasa wa kipato cha chini,”
alisema.
Kuhusu Hospitali ya Mirembe, alisema mafunzo yatatolewa kwa
watumishi ili kukidhi mahitaji ya kutoa huduma kwa waathirika wa dawa za
kulevya na kwa Hospitali ya Bugando kutafungwa CT scan simulator kwa
ajili ya kupanga matibabu na mashine mbili za Varian & Elekta linac
kwa ajili ya matibabu ya saratani.
Hiyo itasaidia matibabu ya mionzi
kutolewa Mwanza badala ya wagonjwa kwenda Dar es Salaam. Ummy alisema
katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC itafungua wodi mpya za wagonjwa
walioungua kwa moto na kemikali na kuanzisha Kitengo cha ICU kwa ajili
ya watoto na kununua vifaa vya uchunguzi vya CT Scan, MRI pamoja na
vifaa kwa ajili ya jengo jipya la huduma za dharura.
Katika hatua
nyingine, waziri amesema serikali imebaini vituo vya afya 73 kati ya
5,235 vilivyopo nchini ndivyo vyenye hadhi ya kuwa vituo vya afya.
Waziri akizungumzia tathmini ya vituo vya afya 5,235, alisema kati yake
vituo 2,016 sawa na asilimia 38.51 vimepata nyota 0, vituo 2,583
vimepata nyota moja, vituo 561 vimepata nyota mbili.
Nyota hizo zote
kuanzia sifuri hadi mbili maana yake havistahili kuwa vituo vya afya. Ni
vituo 68 vilivyopata nyota tatu na vituo vitano vimepata nyota nne
yaani ndiyo vyenye sifa ya kuwa vituo vya afya.
Alisema lengo la
serikali ni kuhakikisha asilimia 80 ya vituo vilivyofanyiwa tathmini
vinapata nyota tatu na zaidi ifikapo Juni mwaka 2018. Alisema wizara
inaangalia uwezekano wa kurekebisha sheria ili kufuta matangazo ya tiba
asili na tiba mbadala.
Alisisitiza kwa wamiliki wa vyombo vya habari
kuhakikisha matangazo yote ya tiba asili na tiba mbadala yanayotolewa
kwenye vyombo vya habari yameidhinishwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba
Mbadala.
Alisema Taasisi ya Taifa ya Utafiti ya Magonjwa wa Binadamu
(NIMR) kwa kushirikiana na kikundi cha kudhibiti Ukimwi Tanga (TAWG)
itafanya majaribio juu ya ubora na usalama wa dawa ya asili aina ya
Tashack ya tiba ya Ukimwi ambayo imeboreshwa na kutengenezwa kiwandani.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuhusu utekelezaji
wa bajeti ya wizara hiyo iliyoomba kuidhinishiwa Sh 845,112,920,056,
Peter Serukamba ameomba serikali kufanyia uchunguzi ongezeko la gharama
kwa baadhi ya maeneo kwa zaidi ya mara 10 katika ujenzi wa jengo la
ghorofa saba la MOI kwa ajili ya kutolea huduma za uchunguzi ikiwemo CT
Scan, MRI, Xray, Ultra Sound, ICU, vyumba vya wagonjwa wanaohitaji
uangalizi wa karibu na vyumba vya wagonjwa wa kulipia na kuchangia.
Jengo
hilo lililokamilika kwa asilimia 95, litakapokamilika litatumia Sh
bilioni 27.23 ambazo ni mkopo kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF).
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment