UTEUZI wa wakuu wa wilaya uliofanywa na Rais John Magufuli, umepongezwa na wengi hasa kutokana na hatua yake ya kuwateua vijana wengi kwamba unafuata falsafa ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Akizungumza na gazeti hili jana, kada mstaafu wa CCM, Pius Msekwa alisema uteuzi ulifanywa na Rais Magufuli ni wa kisayansi zaidi, kwani una lengo la kuwaandaa vijana kurithi uongozi wa nchi kwa siku zijazo.
Msekwa alisema wazee kazi yao kubwa ilikuwa ni kuweka misingi ya nchi na falsafa kubwa ya Mwalimu Nyerere ilikuwa ni kuwataka wazee hao wafahamu kwamba ipo siku watastaafu na nchi lazima ibaki kwa watu ambao wameandaliwa.
“Ndio maana nasema uteuzi wa Rais Magufuli umefuata falsafa hii na ameitekeleza falsafa ya Nyerere, rika iliyoteuliwa ni vijana ambao wameandaliwa kwa ajili ya uongozi wa nchi hii,” alisema Msekwa.
Kuhusu kuwateua wanajeshi katika wilaya za mipakani, Msekwa alisema itasaidia serikali kupata taarifa za kiintelejesia kutoka nchi jirani kama kuna hatari au kuko shwari.
“Serikali inatakiwa kujua mapema hali ya mipakani ikoje, na wanajeshi kwa kutumia mafunzo yao ni rahisi kupata taarifa hizo, hivyo Rais kazingatia vigezo vyote vya msingi,” alisema.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benson Bana aliungana na hoja ya Msekwa kwamba uteuzi wa vijana, una lengo la kuandaa viongozi wa siku zijazo.
Alisema vijana wamepewa nafasi sasa wanatakiwa waoneshe uwezo wao wa kikazi na ubunifu katika kuwatumikia wananchi na kuwaleta maendeleo.
“Mimi siwafahamu wengi walioteuliwa, lakini nasikia wengi ni vijana, hili ni jambo jema kwamba wazee wapumzike wameshafanya mengi kwa nchii na sasa vijana nao waonesha ubunifu wao,” alisema Dk Bana.
Alisema pia kwamba uteuzi huo, una lengo la kuweka watu ambao wataendana na kasi ya Rais Magufuli la kuwatumikia wananchi.
“Rais ana maana kubwa katika uteuzi huu, anataka watu ambao wanaendana na kasi yake,” alisema Dk Bana.
Pia alisema kuwaweka wanajeshi katika wilaya zilizoko mipakani ni jambo jema kwa nchi kwani litasaidia katika masuala ya ulinzi na usalama.
“Hata marais waliopita, hizi wilaya za mipakani mara nyingi wanapelekwa wanajeshi, na hii ni kwa sababu za ulinzi na usalama,” alisema Dk Bana.
Profesa Kitilya Mkumbo alipoombwa kutoa maoni yake kuhusu uteuzi huo alisema, “Mimi siamini kuwepo kwa wakuu wa wilaya, sioni kazi wanazofanya, hivyo naomba nisitoe maoni yoyote kuhusu uteuzi huu.”
Dk Jing John wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema uteuzi wa ma-DC ni muhimu kwa sababu ndio watekelezaji wa maagizo ya serikali katika ngazi za chini za wilaya, hivyo ni lazima rais awe na watu wanaoweza kuendana na kasi yake.
“Rais anataka kuona kile alichoahidi kwa wananchi kinatekelezwa, hivyo uteuzi huu mimi na nauchukuliwa kuwa unaakisi matarajio ya Rais Magufuli,” alisema Dk John.
Alisema Rais anapofanya uteuzi lazima kwanza aone ni watu gani wanaweza kumsaidia kutekeleza ahadi zake alizozitoa kwa wananchi na akasema mchanganyiko wa vijana na wazee ambao Rais ameuweka unaweza kusaidia kutekeleza ahadi hizo.
“Hawa licha ya kusimamia ulinzi na usalama, lakini ndio waratibu na wahamasishaji wa maendeleo, hivyo natarajia watakuwa chachu ya maendeleo kwa kushirikiana na viongozi wengine watakaowakuta huko wilayani,” alisema.
Naye Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Salum alisema Rais kuteua vijana wengi ni jambo jema na alishauri wazee walioachwa wasijisikie vibaya kwani sio kwamba hawafai bali wanaweza kufaa kwa mambo mengine.
“Uteuzi huu hauwezi kuwafurahisha watu wote, kuna watu wana manung’uniko, lakini nashauri tumwache Rais afanye kazi yake maana naamini ameteua watu ambao yeye ana waamini kuwa watamsaidia,” alisema.
Alisema wananchi wanatakiwa kumpa muda Rais waone tija ya wateule wake ao.
“Nimesikia kuna malalamiko kuhusu uteuzi huu, lakini mimi naamini rais ni mwelewa na ana mtazamo wake kuhusu utendaji wa nchi, tumwache atekeleza wajibu wake,” alieleza shehe huyo.
Juzi, Dk Magufuli aliteua wakuu wapya wa wilaya 100 na kuwateua wengine wa zamani 39 na kufanya idadi ya wakuu wote wa wilaya 139. Miongoni mwa hao wapya wamo wakurugenzi watendaji 22 ambao wamepandishwa vyeo na kuwa wakuu wa wilaya.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment