Image
Image

Rais Magufuli amteua Yonazi bosi mpya TSN.

RAIS John Magufuli amemteua Dk Jim James Yonazi kuwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN). Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana ikimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, ilieleza kuwa Rais Magufuli amefanya uteuzi huo kuanzia Juni 18 mwaka huu.
Kabla ya uteuzi huo, Dk Yonazi alikuwa Mkurugenzi wa Menejimenti ya Maarifa katika Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech). Dk Yonazi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Gabriel Nderumaki ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais kuanzia Machi 18, mwaka huu.
Aahidi weledi Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Yonazi amemshukuru Rais Magufuli kwa kumuona anaweza kumsaidia kazi kupitia kampuni hii ya magazeti na kusema amepokea uteuzi huo kwa moyo mkunjufu.
Ameahidi kufanya kazi kwa weledi, kama ambavyo Rais Magufuli amemtaka afanye kuongoza kampuni hii, inayozalisha magazeti ya HabariLeo, HabariLeo Jumapili, Daily News, Sunday News na SpotiLeo.
Alitoa mwito kwa wadau mbalimbali, kushirikiana na TSN kufanya magazeti ya serikali kuwa bora na yenye kuleta changamoto katika tasnia ya habari. Alisema anatarajia kufanya kazi na watu mbalimbali na jambo ambalo anatamani kuona, ni ubunifu, habari za kweli na zinazokwenda na wakati.
Akieleza mtazamo wake kuhusu tasnia ya habari na mambo ambayo analenga kuyafanya baada ya uteuzi, Dk Yonazi alisema wananchi na hata dunia kwa ujumla, ina hamu ya habari za kutoka Tanzania.
Alisema panahitajika ubunifu na mikakati kuhakikisha magazeti ya TSN yanapeleka habari, siyo tu hapa nchini, bali pia kufikia nchi za nje kama ilivyo kwa mashirika ya habari ya kimataifa ya BBC na CNN.
Alisema wakati magazeti ya TSN sasa yanafika nchi za Afrika Mashariki, yanatakiwa kufika pia kwenye masoko ya kanda nyingine na nje ya Afrika. “Tufike mahali, magazeti yawe kwenye viganja vyetu…ningependa sana kufikia hatua hii,” alisema Dk Yonazi, akimaanisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), hususan simu, kutumiwa na wananchi wengi kupata habari.
Alisema anatamani hata watu wa mataifa mengine, waandike habari zao kutoka kwenye magazeti ya nchini hususani ya serikali. Dk Yonazi ni nani? Dk Yonazi ana Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Serikali Mtandao ya Chuo Kikuu Groningen cha Uholanzi na ana Shahada ya Uzamili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama ) na Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Keele, Uingereza.
Amewahi kuwa mhadhiri mwandamizi, mtafiti na mshauri katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dar es Salaam. Pia amefanya utafiti katika masuala mbalimbali kuhusu uvumbuzi, mipango mikakati ya kiutawala katika Tehama.
Aidha, amebobea katika masuala ya mipango ya kiutawala katika Tehama, Uvumbuzi katika Utawala, Serikali Mtandao na Marekebisho ya Sekta ya Umma, Tehama katika Maendeleo na uvumbuzi katika Tehama. Vile vile amehusika katika mikakati mbalimbali ya Tehama hapa nchini na Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).
Pia amewahi kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za kimataifa na za nchini katika ngazi za Umeneja na majukumu makubwa ya usimamizi wa kitaaluma. Dk Yonazi alikuwa Mkurugenzi wa Huduma za Kompyuta katika chuo cha IFM, akisimamia maendeleo katika ugunduzi na ubunifu, iliyowezesha chuo hicho kufanya vizuri katika eneo hilo.
Amewahi kuwa mjumbe wa bodi kadhaa, ikiwamo Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyovunjwa na Rais Magufuli mwishoni mwa Aprili mwaka huu na Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Arusha. Pia ni mjumbe wa Kamati ya Ushauri ya Tehama katika Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) na Mratibu wa Kituo cha Tehama cha Utafiti na Ubunifu (CiRi).
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment