TAIFA linaendelea kugubikwa na majonzi ya mauaji ya Watanzania wenzetu wanane, waliochinjwa na watu wasiojulikana katika Kitongoji cha Kibatini Kata ya Mzizima jijini Tanga usiku wa kuamkia juzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul alithibitisha kwamba watu waliokuwa na visu na mapanga, walivamia kaya tatu usiku wa Mei 30, mwaka huu na kukatisha uhai wa watu hao wanane saa 7.00 usiku.
Taarifa zimefafanua kwamba watuhumiwa hao wa ujambazi, walikuwa wanagonga nyumba ya kaya moja hadi nyingine na kuwatoa kwa nguvu waathirika wa ukatili huo na kisha kuwachinja pasipo chembe ya huruma.
Tunapenda kuungana na Watanzania wenzetu kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa ujumla kwa msiba huu na tunamwomba Mungu azipe subira na nguvu familia zilizoathiriwa na ukatili wa majahili hao.
Tukio hili la mauaji ya watu hao wanane ni mwendelezo wa matukio ya kikatili ya mauaji ya kinyama dhidi ya watu wasio na hatia kwa mwezi ulioisha wa Mei mwaka huu. Tunasema hivyo kwa sababu kumefululiza matukio yapatayo saba katika mwezi mmoja, ambapo watu walichinjwa na kuuawa kwa mapanga na visu katika mikoa ya Mwanza, Tabora, Mara, Dar es Salaam na Tanga.
Hali si shwari. Wakati umefika sasa wa kurejesha utaratibu wa zamani ya kuunda vikundi vya ulinzi wa jadi maarufu Sungusungu katika vitongoji, vijiji na mitaani ili kujihakikishia usalama wetu pamoja na mali zetu.
Hapa tungeomba viongozi wa serikali, wanasiasa, viongozi wa dini na wa kijamii, tuungane katika kuhamasisha kufufua Sungusungu ili tuweze kukabiliana vilivyo na matukio hayo ya kinyama dhidi yetu.
Tunafahamu kwamba vyombo vya dola, ikiwa ni pamoja na majeshi yetu, likiwemo Jeshi la Polisi lenye dhamana ya ulinzi wa raia lipo makini katika kazi zao, lakini ni kweli pia kwamba idadi yao ni ndogo na haliwezi kuwepo kila mahali penye uhalifu wa aina hii.
Sisi tunaamini kwamba kama kungekuwa na Sungusungu, labda unyama uliofanyika kwa hao ndugu zetu wanane waliouawa, huenda usingefanyika kwani uwezekano wa kuwakabili, ungekuwepo kabla hata ya kutafuta msaada kutoka Polisi.
Matukio hayo ya mauaji, yatupe changamoto ya kuhakikisha kwamba viongozi wetu wa ngazi zote za vijiji, vitongoji na mitaa, walivalie njuga suala hili ili vikundi vya Sungusungu vifufuliwe, kutuwezesha kukabiliana kiuhalisia na majahili hao, ambao wanataka kuwajengea hofu Watanzania wasiweze kukabiliana vilivyo na shughuli za za kila siku za kujiletea maendeleo.
Tunapenda kutoa mwito maalumu kwa vyombo vyetu vya dola, kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba waliotekeleza unyama huu wanasakwa, kukamatwa na hatimaye kufikishwa katika vyombo vya sheria ili haki nayo itendeke dhidi yao.
Tunaamini kwamba mshikamano tulionao Watanzania, utatuvusha katika kipindi hiki cha majonzi na kutufikisha katika hali ya kutuwezesha kuweka mikakati thabiti ya kuwadhibiti na kuwatokomeza majahili hao hapa nchini kwetu. Hili linawezekana. Tushikamane.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment