WAKAZI wa Mtaa wa Machinjioni Loliondo (Sagulasagula) waliobomolewa nyumba na Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani kwa tuhuma za kujenga nyumba kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa soko, wamekanusha kupaka kinyesi na kuvunja vioo vya ofisi ya kata ya Maili Moja.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya wenzake, Said Tekelo alisema wao hawahusiki na tukio hilo na wamesikitishwa na kitendo hicho. Bomoabomoa hiyo iliyofanyika Juni 16 na 17 mwaka huu, ilihusisha nyumba 18 na watu hao walidaiwa kufanya uharibifu huo siku moja baada ya bomobomoa hiyo.
Tekelo alisema kitendo hicho kimefanywa na watu ambao walikuwa na malengo yao na hawaungi mkono watu waliofanya uharibifu huo kwani ni tukio ambalo ni kinyume cha sheria na hakistahili kuunga mkono.
“Sisi waathirika wa bomobomoa hii hatuwezi kufanya hivyo kwa sababu bado tuko katika kutafuta haki yetu tuliyoipoteza baada ya nyumba zetu kubomolewa pasipo kupewa fidia yoyote, hivyo hatuwezi kufanya uharibifu wowote,” alisema na kuongeza: “Waliofanya hivyo si miongoni mwetu, sisi hatujashawishi wenzetu kufanya hivyo na waliofanya hivyo wametuharibia sifa yetu kwani hakuna aliyekuwa na akili anaeweza kufanya hivyo,” alisema Tekelo.
Aidha alisema kuwa akili zao zilikuwa katika tafakari ya nini cha kufanya baada ya nyumba zao kubomolewa, huku wakiwa tayari wana malalamiko yao mahakamani na hawakuwa na wazo la kuharibu ofisi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment