CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo kinatarajia kulihutubia
taifa kupitia vyombo vya habari vya ndani na nje kuhusu maazimio ya
Kamati Kuu iliyoketi kwa siku nne mfululizo.
Maazimio
hayo ambayo yanaitwa ‘mazito na makubwa’ kuwahi kutolewa na chama hicho
katika siku za hivi karibuni, yanatarajiwa kuoneshwa moja kwa moja na
vituo vitatu vya runinga nchini.
Chanzo
cha kuaminika kutoka ndani ya chama hicho kimeeleza kuwa maazimio hayo
ya Kamati Kuu yatatangazwa moja kwa moja kupitia baadhi ya vituo vya
runinga kutoa fursa kwa Watanzania kusikiliza maazimio hayo.
Kamati kuu ya Chadema imefanya kikao chake kwa siku nne mfululizo kikiwa kimeghubikwa na usiri mkubwa.
Taarifa
ya chama hicho kwa vyombo vya habari jana, ilisema Kamati Kuu ilimaliza
kikao chake cha siku nne jana na leo maazimio yake yatawekwa wazi kwa
wananchi kupitia vyombo vya habari.
Taarifa
hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema,
Tumaini Makene, ilisema kupitia mkutano huo yatatangazwa maazimio ya
kikao hicho kilichohitimishwa Dar es Salaam jana.
Taarifa hiyo ilisema Chadema kitatoa tamko zito la ukubwa wa aina yake.
“Licha
ya mambo hayo chama kitatoa matamko mazito na makubwa ya aina yake
ambayo hayajawahi kutolewa na chama chetu katika siku za karibuni."
Taarifa
hiyo ilisema Kamati Kuu ilipokea taarifa ya kina juu ya masuala
mbalimbali ikiwa ni pamoja na hali ya siasa nchini kwa sasa ambayo
inatishia hali ya uchumi na ustawi wa jamii nzima kwa ujumla, hivyo
taifa zima kuwa katika majaribu makubwa ya kukosa mwelekeo wa uongozi.
“Kupitia
mkutano huo, Chadema kitatoa mwelekeo wa hali ya nchi hasa wakati huu
ambao taifa linaonekana kukosa dira ya uongozi kwa ajili ya ustawi wa
Watanzania wote kwa ujumla” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka
kuwekwa wazi jina lake.
“Kupitia
mkutano huo, chama kitazungumzia mipango ya kujiimarisha kuendelea
kuwatumikia wananchi na kusimamia dira ya mabadiliko na uhuru wa kweli
nchini,”alisema Makene.
Alipoulizwa
kuhusu taarifa hizo, Makene alisema suala hilo halijathibitishwa rasmi
kama mkutano huo utaonyeshwa moja kwa moja katika runinga.
“Hata
mahali utakapofanyika mkutano huo bado hapajajulikana, nitakupigia simu
kesho asubuhi (leo) kukujulisha wapi tamko hilo litatolewa." Alisema
0 comments:
Post a Comment