Image
Image

'Magereza, JKT ziongeze kasi ya kukamilisha madawati'

RAIS John Magufuli, ameonyesha kutofurahishwa na kitendo cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Magereza cha kutengeneza idadi ndogo ya madawati kutokana na Sh. bilioni nne zilitolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili, mwaka huu.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya madawati hayo jijini Dar es Salaam juzi, Rais Magufuli alieleza kushangazwa kwake na majeshi hayo kutengeneza madawati 53,450 tu kwa miezi mitatu (siku 90) tangu fedha hizo zilipotolewa wakati wana nguvukazi ya kutosha.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilisema katika taarifa kuwa madawati 61,385 ndiyo yaliyotengenezwa hadi juzi katika awamu ya kwanza kutokana na fedha hizo za Bunge.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa madawati mengine 60,000 yatatengenezwa kwenye awamu ya pili.
Rais Magufuli aliongeza kuwa ukigawa idadi ya siku 90 kwa vyombo viwili vya JKT na Magereza, maana yake ni kuwa kila chombo kimetengeneza madawati 30,000.
Rais Magufuli alisema JKT ina kambi nyingi na kwamba ukigawa kwa idadi ya kambi hizo kwa madawati 30,000 unapata wastani wa madawati 30 kwa siku, ambayo yametengenezwa na kila kambi.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wakuu wa JKT na Magereza kuchukua jukumu hilo la utengenezaji madawati kama vita, kwa kuwatumia wafungwa na nguvukazi iliyoko katika vikosi kuharakisha utengenezaji wa madawati.
Rais Magufuli alikuwa na kila haki ya kuonyesha kutoridhishwa na kasi ndogo ya utengenezaji wa madawati hayo, kwa sababu taasisi hizo mbili za serikali sio tu zina nguvukazi ya kutosha pekee wakiwamo wafungwa na askari, lakini pia zina uwezo mkubwa wa kutengeneza madawati yenye ubora kulinganisha na kampuni binafsi.
Kama alivyosema kwamba suala la madawati ni vita, waliopewa jukumu hilo walipaswa kuelekeza nguvu zao kuhakikisha kazi hiyo inakamilika haraka sana kwa kuzingatia kuwa shule nyingi za umma zimeshafunguliwa na chache zonaendelea kufunguliwa.
Sababu nyingine ambayo ilipaswa kuwasukuma Magereza na JKT kukamilisha kazi hiyo haraka ni kutokana na mwitikio mkubwa wa taasisi za umma, asasi na watu binafsi katika kuchangia madawati, lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli la kumaliza tatizo kubwa na la muda mrefu la madawati nchini.
Tunaamini kuwa kwa kuwa kauli yake imesikika, kilichobaki sasa ni wahusika kuichukulia kama changamoto kwao na kujipanga upya kisha kuikamilisha kazi hiyo mapema iwezekanavyo.
Upo msemo wa Kiswahili kuwa kujikwaa siyo kuanguka, tukiwa na maana kuwa wahusika hawajashindwa kutekeleza kazi hivyo, hivyo wataikamilisha kama ilivyotarajiwa kwa kuzingatia kuwa ni taasisi ambazo zimeaminiwa na Serikali na kupewa zabuni hiyo.
Kwa kuwa ombi la mkubwa huwa ni amri, tunaamini kuwa kazi hiyo sasa wataifanya usiku na mchana kuhakikisha inakamilika na watoto wetu wengi wanaanza kukalia madawato. Hayo ndiyo mabadiliko ya kweli ambayo Serikali ya Awamu ya Tano iliahidi kuletea Watanzania.
Licha ya kasi kubwa ya upatikanaji wa madawati, bado changamoto zinatendelea kujitokeza kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa, hali inayochangiwa na kufutwa kwa ada katika shule za msingi na sekondari.
Kutokana na hali hiyo, tunatoa wito kwa jamii nzima kutambua kuwa ajenda ya kuchangia madawati hainabudi kuwa endelevu na kila mmoja anatakiwa kushiriki.

    Share on Google Plus

    Kuhusu TAMBARARE HALISI

    This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

    0 comments:

    Post a Comment