Image
Image

Serikali yawatumbua Wakala wa Misitu na wengine 41 kuhamishwa vituo vya kazi.


SERIKALI imemuondoa katika nafasi yake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Gerald Kamwenda na wakurugenzi wenzake, katika jitihada za kufumua na kusuka upya shirika hilo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, ametangaza hatua hiyo ya serikali jana alipokutana na vyombo vya habari na kuongeza kuwa, watumishi wengine 41 wamehamishwa vituo vya kazi.
Alifafanua kuwa hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, lililotaka kufumuliwa na kusukwa upya kwa TFS ili kuongeza ufanisi.
Kutokana na hatua hiyo, Waziri Maghembe alisema Profesa Dos Santos Silayo ameteuliwa kuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa TFS, wakati Kamwenda anahamishiwa Chuo cha Viwanda vya Misitu kilichopo Moshi.
Aidha, Mwanaidi Kijazi aliyekuwa Mkurugenzi wa Usimamizi wa Raslimali za Misitu na Nyuki, yeye amekwenda kuwa Mhifadhi Mkuu Amani Nature Reserve na nafasi yake inachukuliwa na Zawadi Mbwambo.
Waziri Maghembe alisema Mohamed Kilongo aliyesimamishwa kazi Januari 5, mwaka huu uchunguzi umeonekana hana hatia na hivyo anaendelea kuwa Mkurugenzi Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu.
Alisema Wizara imeamua Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Gladnes Mkamba ahamishiwe Idara ya Mipango makao makuu na nafasi hiyo kuteuliwa Dk Ezekiel Mwakalukwa, kuwa Kaimu Mkurugenzi.
Aidha Monica Kagya aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Ufugaji Nyuki, anakuwa Mtafiti Mwandamizi Idara ya Nyuki (Tawiri). Alisema Kagya ni mtaalamu wa masuala ya nyuki, hivyo atahamishiwa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori, ili ashughulikie utafiti wa masuala ya nyuki.
Pia alisema katika Idara ya Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa anakuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, nafasi ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Herman Kerayo ambaye anahamishiwa Idara ya Mipango Makao Makuu.
Profesa Ramadhan Kideghesho, yeye anakwenda kuwa Mkuu wa Chuo cha Mweka wakati Mabula Misungwi aliyekuwa Meneja Mradi Selous, anakwenda Chuo cha Wanyamapori Pasiansi na nafasi yake inachukuliwa na Jaffary Lyimo, huku Robert Mande akipelekwa kuwa Kaimu Mkurugenzi msaidizi Uzuiaji Ujangili.
Waziri Maghembe alisema Majjid Ally ameteuliwa kuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Leseni, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Haji Mpya ambaye amehamishiwa Shamba Jipya Songea kuwa Ofisa Misitu Alisema Julai 18, mwaka huu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikutana na viongozi na watumishi wa Wizara hiyo na watendaji wakuu na watumishi wa TFS na kuagiza kufumuliwa na kusukwa upya kwa wakala huo.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu alitaka kuondolewa kwa utitiri wa vituo vya ukaguzi na kuwekwa vituo vichache na kuondolewa kwa ofisi za makontena yanayotumiwa na ofisi ya TFS, badala yake watumishi wanaofanya ukaguzi wasimame mahali pa wazi ili kuondoa mianya ya rushwa na kuweka uwazi katika utendaji.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment