TAASISI
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imewatia mbaroni wamiliki
na wafanyakazi wa kampuni kadhaa zinazodaiwa kukwepa kodi kwa
kutengeneza stakabadhi feki.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya
Rais Dk. John Magufuli, kueleza habari za mfanyabiashara mmoja ambaye
amekuwa akifanya miamala ya fedha inayofikia Sh milioni saba hadi nane
kwa kila dakika moja na hivyo kuikosesha Serikali mapato.
Pamoja na
hatua hiyo, habari zaidi zinaeleza kuwa taasisi hiyo pia imebaini uwepo
wa kampuni zaidi ya 300 ambazo zinahusika katika mchezo huo mchafu.
Kampuni
hizo zimetakiwa kulipa takribani zaidi ya Sh bilioni 30, ambazo
zinaelezwa kuwa zimeibwa kupitia mtindo huo wa kudurufu stakabadhi
bandia zenye nembo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Taarifa za
uhakika ambazo MTANZANIA ilizipata tangu juzi jioni, zinaeleza kuwa
watendaji wa Kampuni ya Farm Plant (T) Limited, wamekamatwa na TAKUKURU
kwa uchunguzi zaidi.
“Ni kweli watendaji wa juu wa Farm Plant
wamekamatwa na Takukuru, wapo watatu na kwa sasa wamehifadhiwa katika
kituo cha Polisi Magomeni kwa uchunguzi zaidi. Na huenda kesho (leo)
wakafikishwa mahakamani,” kilisema chanzo chetu cha kuaminika.
MTANZANIA
ilipomtafuta Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Benn Lincolin,
simu yake iliita bila majibu hadi tunakwenda mitamboni.
Hata hivyo watuhumiwa hao kwa sasa tunawahifadhi majina kutokana na sababu za kitaaluma.
Pamoja
na hali hiyo taarifa kutoka mkoani Iringa zinaeleza kuwa Jeshi la
Polisi lilimtia mbaroni mmoja wa viongozi wa kampuni iliyotajwa kukwepa
kodi na kutengeneza stakabadhi bandia.
Chanzo cha uhakika kililiambia
gazeti hili kuwa mfanyabishara huyo alitiwa nguvuni Jumamosi, ambapo
jana alisafirishwa hadi jijini Dar es Salaam kuungana na watuhumiwa
wengine ambao wote huenda wakafikishwa mahakamani leo.
MTANZANIA
ilipomtafuta Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna Valentino Mlowola ili
kupata ufafanuzi wa kukamatwa kwa watuhumiwa hao, alisema hawezi
kuzungumzia suala hilo hadi atakapopata taarifa kutoka kwa watendaji
wake.
“Unajua leo (jana) ni siku ya mapumziko ninachokuomba vuta
subira kesho (leo) kwa kuwa ni siku ya kazi njoo ofisini nitakueleza
taarifa zote. Maana kuna timu ya watendaji ndiyo wanashughulikia nami
nitazungumza hadi pale nitakapopata taarifa hizo,” alisema Kamishna
Mlowola.
Wiki iliyopita wakizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam, Mlowola pamoja na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), Alphayo Kidata, walieleza jinsi kampuni hizo feki zilivyoiibia
Serikali kupitia stakabadhi za mfumo wa kielektroniki (EFD’s).
Kamishna
Kidata, alisema kampuni hizo zimekuwa zikinunua stakabadhi za manunuzi
bandia kutoka kwa watu wanaomiliki mashine za kielektroniki ambazo
hazijasajiliwa na kuzitumia na kisha kudai marejesho ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) bila kuwapo na bidhaa au stakabadhi halali
iliyouzwa au kutolewa na muhusika.
Alisema TRA kwa kushirikiana na
Takukuru bado wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kampuni zote
zinazojihusisha na mchezo huo mchafu wa kuiibia Serikali.
Mtendaji
huyo wa TRA alisema hadi sasa tayari wamezibaini kampuni nne ambazo
zimekuwa zikijihusisha na ukwepaji kodi kwa mtindo huo tangu mwaka 2010
hadi 2014 na kupoteza mapato ya Serikali kiasi cha Sh bilioni 29.2.
Alizitaja
kampuni hizo kuwa ni Skol Building Material Ltd, ambayo imebainika
tangu mwaka 2012 hadi 2013 haikulipa VAT ya Sh bilioni 5.4 na kodi ya
mapato yenye thamani ya Sh bilioni 10.9, hivyo kudaiwa jumla ya Sh
bilioni 16 kwa kipindi hicho.
Kampuni nyingine ni Farm Plant (T) Ltd,
ambayo alisema tangu mwaka 2010 hadi 2014 haikuwahi kulipa VAT ya jumla
ya Sh bilioni 5 na kodi ya mapato yenye thamani ya Sh bilioni 4 ambayo
ni jumla ya kodi inayodaiwa kufikia Sh bilioni 9.
“Kampuni nyingine
ni A. M Trailer Manufacturers Ltd ambayo tangu mwaka 2013 hadi 2014
haikuwahi kulipa VAT ya Sh bilioni 6 na kodi ya mapato yenye thamani ya
Sh bilioni 1 ambayo jumla ya fedha inazotakiwa kurejesha ni Sh bilioni
1.7.
“Baada ya kubaini ukwepaji kodi wa makampuni haya, TRA kwa
kushirikiana na Takukuru inaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo na baada
ya uchunguzi kukamilika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya
watakaobainika kukwepa kodi,’’ alisema Kidata.
Kutokana na hali hiyo,
alitoa wito kwa wafanyabiashara kutojihusisha na kununua stakabadhi
bandia, na kudai marejesho ya VAT yasiyostahili kwa kuwa mamlaka
imejizatiti kuendelea kuwabaini wakwepa kodi wote.
Kuhusu baadhi ya
wafanyakazi wa TRA kujihusisha na mtandao huo wa kudurufu mfumo wa
kukwepa kodi na kuiibia Serikali, alisema wanaendelea na uchunguzi na
kama wapo nao watachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake,
Kamishna Mlowola, alisema uchunguzi bado unaendela kwa kampuni 300
ambazo zimetakiwa kulipa fedha hizo na wakishindwa watafikishwa
mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Pamoja na hali hiyo, alisema
mfanyabiashara huyo aliyebainika kuwa na makampuni mengi, alikuwa
akishirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA)
pamoja na TRA.
Mtandao mpana
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa
mtandao wa wafanyabiashara hao ambao wamekuwa wakiibia Serikali, upo kwa
makampuni zaidi ya 20,000 ambazo zimekuwa zikiendesha mchezo huo mchafu
tangu 2010.
Chanzo cha kuaminika kililiambia MTANZANIA kuwa kwa wiki
moja sasa vyombo vya dola vimekuwa vikipambana na mtandao huo ambapo
inaelezwa kuwa vinara hao tayari wapo katika mikono salama.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment