BODI
ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) imeagiza
kusimamishwa kwa wakurugenzi sita, mameneja watano na mhandisi mmoja wa
shirika hilo kupisha uchunguzi, kubaini wahusika katika tuhuma za
ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na
taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na
ajira.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Profesa Samwel
Wangwe, alikiri katika mazungumzo na gazeti hili jana usiku kusimamishwa
kwa vigogo hao 11, kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizoelekezwa kwao.
“Ni
taarifa sahihi hizo. Kulikuwa na tuhuma katika ripoti ya ukaguzi, kwa
hiyo tumeamua wakae pembeni ili kupisha uchunguzi, hawajafukuzwa kazi.
Taarifa hiyo ya kusimamishwa ni sawa sawa,” alisema Profesa Wangwe jana
usiku.
Kwa mujibu wa taarifa kwa wafanyakazi, iliyotolewa na Ofisi ya
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, iliwataja wakurugenzi sita waliosimamishwa
kuwa ni Yacob Kidula (Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi),
Ludovick Mrosso (Mkurugenzi wa Fedha) na Chiku Matessa (Mkurugenzi wa
Rasilimali Watu na Utawala).
Wengine ni Sadi Shemilwa (Mkurugenzi wa
Udhibiti Hadhara na Majanga), Pauline Mtunda (Mkurugenzi wa Ukaguzi wa
Mahesabu ya Ndani) na Crescentius Magori (Mkurugenzi wa Uendeshaji).
Aidha,
taarifa hiyo iliwataja mameneja waliosimamishwa kuwa ni Amina Abdallah
(Meneja Utawala), Abdallah Mseli (Meneja wa Uwekezaji), Mhandisi John
Msemo (Meneja wa Miradi), Davis Kalanje (Mhasibu Mkuu), Wakili Chedrik
Komba (Meneja Kiongozi – Mkoa wa Temeke) na Mhandisi John Ndazi (Meneja
Mradi).
Taarifa hiyo kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, ilisema
kwamba uamuzi huo umefanywa na Bodi chini ya Profesa Wangwe iliyokutana
Julai 15, mwaka huu kutokana na taarifa mbalimbali za wakaguzi wa
hesabu na shughuli za uendeshaji wa shirika hilo la umma.
“Bodi ya
Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii chini ya Uenyekiti wa
Profesa Samwel Wangwe katika kikao chake cha 106 kilichofanyika tarehe
15 Julai, 2016 kimeagiza kusimamishwa kazi kwa wakurugenzi sita (6),
mameneja watano (5) na mhandisi mmoja ili kupisha uchunguzi kubaini
wahusika katika tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na
kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa
miradi na manunuzi ya umma na ajira,” ilieleza taarifa hiyo.
Hivi
karibuni, NSSF ilitajwa katika vyombo vya habari kuhusu tuhuma zikiwamo
za ununuzi wa ardhi usiofuata taratibu za manunuzi ya umma, kuwapo kwa
ubadhirifu na ajira za upendeleo katika shirika hilo, ukiwataja wahusika
kuwa ni baadhi ya wakurugenzi wa shirika hilo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment