KILA kukicha Watanzania wanapenda kusikia habari za mchezaji wao wa
kimataifa, Mbwana Samatta, ambaye anakipiga katika klabu ya Genk ya
nchini Ubelgiji.
Huyu ni mchezaji pekee ambaye anaipeperusha vema bendera ya Taifa kutokana na jitihada zake za kutaka kucheza soka barani Ulaya.
Kujiamini kwake kumemfanya atimize ndoto zake, inawezekana kuwa bado
hazijatimia lakini Watanzania wengi wanaamini ndoto zake zimetimia.
Kwa maelezo ya Samatta ni kwamba, ndoto zake aje kucheza soka la kimataifa hasa katika Ligi Kuu nchini England.
Dalili za kutimia kwa ndoto zake zinaanza kuonekana kwa kuwa mchezaji
huyo hadi sasa anaonesha uwezo wa hali ya juu katika msimu mpya wa Ligi
Kuu nchini Ubelgiji, huku klabu yake ikishika nafasi ya tano kwenye
msimamo wa ligi baada ya kucheza michezo minne.
Katika michezo hiyo ambayo amecheza, nyota huyo anaongoza kwa
ufungaji huku akiwa na mabao 3 katika michezo hiyo aliyocheza, wakati
huo anapambana na wapinzani wake watatu ambao wote wana mabao matatu
kila mmoja, nyota wa Mouscron ambaye anajulikana kwa jina la Filip
Markovic, Jeremy Perbe wa Gent na David Pollet wa klabu ya Charleroi.
Samatta alivyoanza kuitumikia klabu ya Simba SC ya nchini Tanzania
wala hakuwa na haraka kwa kuwa alikuwa anajua nini anakifanya akiwa
uwanjani.
Katika michezo yake ambayo alicheza tangu asajiliwe na klabu hiyo
alionesha uwezo wake mkubwa na kuwashawishi klabu ya TP Mazembe ya
nchini Congo kuweza kufanya naye mazungumzo kwa ajili ya kumsajili.
Hata baada ya Mazembe kumsajili mchezaji huyo pia alionesha uwezo
wake wa hali ya juu huku akiwa na lengo la kutaka kusonga mbele katika
ligi kubwa hasa barani Ulaya.
Hata hivyo, amefanikiwa kufanya hivyo japokuwa bado kuonekana katika
ligi ya nchini England, lakini kuna uwezekano mkubwa wa msimu ujao
kupata timu nchini humo kama ataendelea na kazi yake ya kujituma na
kupachika mabao.
Lakini kwa wachezaji wengine wa hapa nchini akili zao ni kuja kucheza
soka katika klabu ya Simba, Yanga na Azam FC, lakini si wengi ambao
wanafikiria kuja kucheza soka la kulipwa barani Ulaya kama ilivyo kwa
Samatta.
Ninaamini kama wapo wachezaji wengi ambao wana mawazo kama Samatta,
basi soka letu lingebadilika na lingekuwa na ushindani wa hali ya juu
kwa kuwa wangeonesha uwezo mkubwa hasa pale wanapokutaka na timu
nyingine za mataifa mbalimbali.
Ninatamani kuona siku moja kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa
Stars’ akiita kikosi chake huku wachezaji mbalimbali wakiwa wanatoka
katika klabu kubwa barani Ulaya na sehemu nyingine na kuungana pamoja
kwa ajili ya kuja kulisaidia taifa lao.
Lakini wachezaji hawa ambao wanacheza Ligi Kuu nchini Tanzania
wakiendelea kufikiria kucheza soka katika klabu ya Simba, Yanga na Azam,
basi tutashindwa kufanya vizuri kimataifa kama watashindwa kujituma na
kupata nafasi ya kucheza soka nje na kupata changamoto mpya. Ni vizuri
wachezaji wetu wakawa na wivu kwa mafanikio ya Samatta na wawe na lengo
la kwenda kucheza soka nje, inawezekana kama watakuwa tayari na kujitoa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment