Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza
viongozi wote wa kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Kitongoji nchini mwake
kufuatilia matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kutoa
elimu bila malipo kwa lengo la kudhibiti mianya ya matumizi mabaya ya
fedha hizo.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo katika mkutano wa
hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mnadani na kuwajumuisha wananchi wa
Katoro na Buseresere Mkoani Geita.
Katika agizo hilo Dkt. Magufuli
amewaonya walimu ambao wameanza kufanya udanganyifu kwa kuandikisha
idadi kubwa ya wanafunzi kuliko idadi halisi kwa lengo la kupata mgao
mkubwa wa fedha za ruzuku na amesema Serikali itachukua hatua kali dhidi
ya yeyote atakayebainika kufanya hivyo.
"Ninafahamu mgao wa fedha
hizo hutolewa kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo, wapo baadhi ya
walimu ambao wameanza kuandika wanafunzi hewa katika shule zao, ili
kusudi aletewe hela nyingi kuliko idadi ya wanafunzi waliopo, wanafunzi
kama wapo laki nne yeye anasema shule yangu hii ina wanafunzi laki tano,
ili kusudi hela zikija za wanafunzi laki tano, za wanafunzi laki moja
wagawane.
"Napenda nitoe wito kwa walimu Tanzania nzima, mnatafuta
matatizo, narudia mnatafuta matatizo, msijaribu kula hela ya Serikali"
Amesema Rais Magufuli.
Pamoja na agizo hilo, Rais Magufuli pia
ametaka viongozi wa ngazi zote katika Mikoa kuhakikisha wana takwimu za
idadi ya wanafunzi katika shule zote zilizopo katika maeneo yao ili
kurahisisha ufuatiliaji wa fedha hizo na amesema kuwa kuanzia sasa
ataanza kutembelea shule kwa kushitukiza na kwamba kiongozi
atakayeonekana kutojua takwimu itakuwa ni uthibitisho kuwa hatoshi
kuendelea na wadhifa alionao.
"Na nitoe wito kwa viongozi wa Mikoa,
Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Makatibu Tarafa, Watendaji
wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji, kila mmoja awe na idadi ya wanafunzi
waliopo katika shule zao, hatutaki kuwapunja wanafunzi hela ambayo
wanatakiwa kupata, lakini pia hatutaki kutoa hela ambayo haitakiwi"
Amesisitiza Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ametumia mkutano
huo kueleza juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali yake ya Awamu ya
Tano, kutekeleza ahadi yake ya kujenga Tanzania Mpya pia amewataka
viongozi na watendaji wa Serikali kutekeleza wajibu wao kwa kutembelea
wananchi wanaowaongoza badala ya kukaa muda mwingi ofisini huku
akisisitiza ofisi hizo kuwepo katika maeneo yenye shughuli husika.
Aidha,
Dkt. Magufuli amekosoa utaratibu unaotumiwa na Halmashauri nyingi za
Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya kutumia mawakala katika ukusanyaji wa
mapato ya Halmashauri akisema mawakala hao wamekuwa wakitumia utaratibu
huo kukusanya fedha nyingi na kisha kuwasilisha kiasi kidogo katika
Halmashauri husika.
"Hivi kwa nini Halmashauri msingekuwa na maafisa
wenu wazuri na mkawa na mashine za kielektroni kwa ajili ya kukusanya
fedha? Amehoji Dkt. Magufuli na kuongeza kuwa "tena mawakala wengine
ndio hao hao wamekuwa wakikusanya kodi hata kwa wananchi wanyonge wenye
vibiashara vidogo vya kuuza mchicha bila hata kuwaonea huruma"
Rais
Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amemaliza
ziara yake ya siku nne katika Mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na
Geita na yupo nyumbani kwake Chato Mkoani Geita kwa mapumziko mafupi.
Home
News
Slider
Magufuli acharuka, awapiga mkwala walimu wanaoandikisha wanafunzi hewa ili kupata mgao.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment